Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Michael Mwang'onda (kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (kushoto mwenye skafu) wakifurahia uwekaji jiwe la msingi wa jengo la mama na mtoto katika kituo cha afya Magoto kata ya Nyaikonga mradi unaogharamiwa na Barrick North Mara.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang’onda, akikagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyofadhiliwa kupitia fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR) za Barrick North Mara katika Wilaya ya Tarime.
.jpeg)
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Matongo wakishuhudia uzinduzi wa vyumba vipya vya madarasa vya CSR ya Barrick North Mara.

Meneja Msaidizi wa Idara ya Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Nasieku Kisambu akipokea Mwenge wa Uhuru wakati wa uzinduzi wa miradi ya CSR inayotekelezwa na mgodi huo.
*****
👉Miradi zaidi ya CSR ya elimu na afya yazinduliwa mbio za mwenge 2026
Kupitia utekelezaji wa mkakati endelevu wa kampuni na sera za serikali kwa weledi, mgodi wa Barrick North Mara uliopo wilayani Tarime unaendelea kufanikisha miradi mbalimbali kupitia fedha za uwajibikaji wa jamii (CSR), hususani katika sekta ya afya na elimu katika vijiji vinavyozunguka mgodi. Mbio za Mwenge wa Uhuru zinazoendelea mkoani Mara zimezindua baadhi ya miradi iliyotekelezwa katika kata mbalimbali.
Miradi ya Barrick North Mara iliyozinduliwa na Mbio za Mwenge 2026 ni ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Matongo na ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto katika Kituo cha Afya Magoto kilichopo Kata ya Nyakonga, ambayo imetekelezwa na wakandarasi wazawa. Miradi hiyo yote imegharimu kiasi cha shilingi milioni 293.5.
Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa Mgodi wa North Mara umetumia shilingi bilioni 26.86 kugharamia utekelezaji wa miradi ya CSR 255 katika sekta za elimu, afya, barabara, maji, miradi ya kiuchumi na mazingira katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime tangu mwaka 2019 ulipokabidhiwa kwa Barrick.
Akiongea mara baada ya kukagua na kuzindua mradi wa vyumba viwili vya madarasa, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang’onda, ameipongeza Kampuni ya Barrick kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.
.jpeg)
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang’onda, akizungumza wakati wa uzinduzi wa miradi ya CSR ya Barrick North Mara wilayani Tarime.
Mwang’onda amesema ushirikiano kati ya serikali na wadau wa maendeleo unaendelea kuzaa matunda chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameweka mazingira mazuri ya uwekezaji yanayowezesha sekta binafsi kushiriki katika kuchochea maendeleo ya wananchi.
“Namshukuru Rais Samia kwa jinsi ambavyo anajenga mahusiano mazuri na wadau wa maendeleo, kwani hapa tunashuhudia wadau wetu wa maendeleo Barrick, wakifanya kazi kubwa kwa kushirikiana na serikali,” amesema.
Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru amesema fedha zilizowezesha ujenzi wa madarasa hayo ni sehemu ya mapato ambayo Barrick inairejesha kwa jamii kutokana na shughuli zake za uchimbaji madini nchini.
“Barrick wametoa fedha ambayo wanarudisha kwa serikali kutokana na shughuli wanazofanya katika nchi yetu. Tunawashukuru sana kwa kazi kubwa ambazo wanazifanya, tumeambiwa hapa pia kuna jengo la utawala na maabara, wamefanya kazi kubwa kwa kushirikiana na serikali,” amesema.
“Namshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyoendelea kuboresha sekta ya elimu nchini. Hata wanafunzi wetu hawa wanasoma bure kuanzia elimu ya msingi,” amesema Mwang’onda.
Akihitimisha mazungumzo yake kwenye mradi huo wa elimu, Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru amesema Mwenge wa Uhuru umevutiwa na ubora wa mradi huo na kuridhishwa na namna ulivyotekelezwa.
“Niseme tu kwamba Mwenge wa Uhuru umefurahishwa sana na ujenzi wa vyumba hivi vya madarasa na uko tayari kuvizindua,” amesema Mwang’onda na kupigiwa makofi na mamia ya wananchi waliojitokeza kushuhudia tukio hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Shule ya Sekondari Matongo, Mwalimu Zablon Obuya Orege, mradi huo ulianza kutekelezwa Juni 21, 2025 na kukamilika Juni 29, 2026.
“Hadi sasa mkandarasi aliyetekeleza mradi huu amelipwa kiasi chote cha shilingi 63,800,000,” amesema Mwalimu Orege na kuishukuru serikali kwa jitihada za kushirikiana na sekta binafsi kujenga na kuboresha miundombinu ya elimu.
Amebainisha kuwa utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya jitihada za kujiandaa kikamilifu kwa mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2028 ili kuendana na mabadiliko ya Sera ya Elimu nchini.
Akiwa kwenye mradi wa ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto katika Kituo cha Afya Magoto, Kata ya Nyakonga, Mwang’onda pia amefurahishwa na utekelezaji wa mradi huo ambao utagharimu shilingi zaidi ya milioni 200 hadi kukamilika kwake.
“Mwenge wa Uhuru umefika na kukagua mradi wa jengo la mama na mtoto hapa Nyakonga na unaendelea vizuri. Wadau hawa wa Barrick wanafanya kazi kubwa na tunawashukuru sana kwa kurudisha sehemu ya faida yao katika jamii,” amesema.
Miradi hiyo ni sehemu ya miradi mipya 103 ambayo inatekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime chini ya mpango wa CSR Barrick North Mara.
Mwang’onda amesema Rais Samia Suluhu Hassan anaendelea kuleta mageuzi makubwa ya uboreshaji wa sekta ya afya, ikiwemo huduma kwa wajawazito.
Amesema serikali inaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya afya katika halmashauri zote nchini.
“Rais Samia anapeleka huduma za afya karibu na wananchi, hataki kuona wananchi, hasa akina mama wakisafiri umbali mrefu, anapeleka majengo ya mama na mtoto kila sehemu, lengo kubwa ni kuona wanajifungulia katika maeneo ya karibu, siyo kusafiri umbali mrefu.
“Rais Samia haishii kujenga majengo tu, anapeleka vifaa tiba vya kisasa, akina mama sasa hivi hawahangaiki, hata ukienda zahanati unakuta vifaa tiba vya kisasa,” ameongeza Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Mwang’onda amesema uwekezaji wa mabilioni ya fedha za CSR kutoka kampuni ya Barrick inayomiliki migodi ya dhahabu ya North Mara na Bulyanhulu kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals ni ushahidi wa matunda ya sera nzuri ya uwekezaji iliyopo nchini.
Ameihakikishia Barrick kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wanaoshirikiana na wananchi katika kuleta maendeleo, huku akiitaka kampuni hiyo kuendeleza mchango wake katika sekta za kijamii.
“Endeleeni kushirikiana na serikali yetu inawapenda sana na iko tayari kuwawekea mazingira rafiki ili muendelee kuchapa kazi katika taifa letu, endeleeni kufanya kazi, mko kwenye mikono salama ya Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesisitiza.
Kwa upande mwingine, Mwang’onda amewapongeza viongozi wa Wilaya ya Tarime na Mkoa wa Mara kwa ushirikiano wao na sekta binafsi, akisema juhudi hizo zimekuwa chachu ya utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa wananchi.
“Nishukuru viongozi kwa kazi kubwa mnayofanya kwa kushirikiana na wadau hawa wa maendeleo, endeleeni kufanya hivyo kwani serikali yetu inategemea sana sekta binafsi,” amesema Mwang’onda.
Mwang’onda ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi wa Tarime kuendelea kulinda amani na utulivu, akieleza kuwa mazingira hayo ndiyo msingi wa maendeleo endelevu ya jamii.
“Nawaomba sana wananchi kuendelea kulinda amani na utulivu ili nchi yetu iendelee kubaki tulivu viongozi wetu wakiongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan waendelee kuiletea maendeleo makubwa zaidi.
“Ndugu zangu wana-Tarime, palipo na amani ndipo penye maendeleo,” amesisitiza Mwang’onda.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, amesema miradi ya CSR Barrick North Mara imetapakaa katika halmashauri hiyo.
“Miradi ya CSR ipo katika kata 26, na kwenye sekta za afya, elimu, maji na barabara. CSR imepunguza hata mzigo kwa wananchi kuchangia miradi,” amesema Waitara.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Matongo, Charles Ryoba, amesema miradi ya CSR Barrick North Mara imeisaidia jamii.
“Kwa mfano Shule ya Sekondari Matongo, asilimia zaidi ya 90 ya majengo yake yamejengwa kutokana na fedha za CSR Barrick North Mara. Barrick ina vitu ambavyo imejenga Matongo, ndiyo maana mahusiano yanazidi kuimarika,” amesema Ryoba.







Social Plugin