Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC NDILE :VUTENI SUBIRA MSIWAUZIE WALANGUZI MAHINDI

Zao la mahindi  linalolimwa Mkoani Ruvuma ambalo wakulima wakisubiria bei elekezi ya Serikali ya ununuzi wa zao hilo 
Mkuu wa Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Wilman Kapenjama Ndile Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu bei elekezi inayotarajiwa kutangazwa wiki ya pili ya mwezi agosti mwaka huu na kuwaomba wakulima kuwa na subira wakati wakisubiri Serikali kutangaza bei elekezi ya ununuzi wa zao hilo la mahindi

Na Regina Ndumbaro

Songea-Ruvuma 

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Wilman Kapenjama Ndile, amewataka wakulima wa mahindi kuwa na subira wakati wakisubiri Serikali kutangaza bei elekezi ya ununuzi wa zao hilo, akisisitiza wasikimbilie kuwauzia walanguzi. 

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Ndile amesema Serikali inatarajia kutangaza bei hiyo katika wiki ya pili ya Agosti 2026, hivyo amewashauri wakulima wenye mahitaji ya kifedha kuuza mazao mengine kama maharage, soya na mbaazi ili kujikimu badala ya kuuza mahindi kwa bei ya hasara. 

Amesema kadri mkulima anavyoweza kuhifadhi mahindi yake ndivyo anavyoongeza nafasi ya kupata bei nzuri zaidi.

Ndile pia amefafanua kuhusu ushuru wa shilingi 1,000 kwa kila gunia la mahindi unaotozwa katika maeneo ya ununuzi, akieleza kuwa ni kodi halali inayokusanywa na Halmashauri na hutumika kugharamia huduma za maendeleo kama ukarabati wa zahanati, shule na nyumba za walimu. 

Amesema katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea pekee, mapato yatokanayo na ushuru huo yanaweza kufikia kati ya shilingi milioni 700 na 800 kwa mwaka, fedha ambazo hurejeshwa kwa wananchi kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amelaani vitendo vya baadhi ya wakusanyaji wa ushuru wanaowatoza wananchi wenye magunia machache ya mahindi wanaposafirisha mazao yao kutoka vijijini ametolea mfano kama Litisha na Kilagano kwenda maeneo mengine, akisisitiza kuwa maelekezo ya Serikali yanazuia kutozwa ushuru kwa anayesafirisha magunia yasiyozidi tisa au mazao yasiyofikia tani moja kwa matumizi ya nyumbani. 

Amesema wananchi wanaosafirisha mahindi kwa matumizi yao binafsi wanapaswa kuwa na barua ya utambulisho kutoka kwa mwenyekiti wa kijiji na hawapaswi kulipa ushuru, huku akionya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watumishi watakaoendelea kuwanyanyasa wananchi. 

Hata hivyo, amesisitiza kuwa wanaobainika kugawa makusudi mizigo mikubwa katika safari ndogo ndogo ili kukwepa ushuru nao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Katika hatua nyingine, Ndile ametangaza namba yake ya simu 0768 077 777 kwa ajili ya wananchi kutoa taarifa za dhuluma, uonevu na changamoto mbalimbali zinazowakabili saa 24 kwa siku, huku akiwaonya wasiitumie vibaya kwa kupiga simu zisizo na sababu za msingi. 

Pia amewatahadharisha madalali wanaouza mifuko ya NFRA, akieleza kuwa mifuko hiyo hutolewa bure katika vituo vya ununuzi wa mahindi na yeyote atakayebainika akiichuuza au kuwatoza wananchi fedha atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com