Na mwandishi wetu Arusha.
Zaidi ya wananchi 8,000 kutoka Mkoa wa Arusha na maeneo mengine nchini wamepata huduma za uchunguzi na matibabu bila malipo katika siku mbili za kwanza za kambi maalumu ya afya inayofanyika jijini Arusha.
Kambi hiyo ya siku saba ilianza Jumatatu, Julai 13, 2026, na inatarajiwa kufungwa Jumapili, Julai 19, 2026. Katika kipindi hicho, wananchi wanapatiwa vipimo, ushauri wa madaktari bingwa, matibabu, dawa na rufaa bila malipo.
Kambi imeandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Mheshimiwa Paul Christian Makonda, pamoja na Wizara ya Afya, hospitali za rufaa za kitaifa, taasisi maalumu za afya na hospitali binafsi.
Katika siku ya kwanza, Jumatatu, Julai 13, wananchi 3,500 walipata huduma kamili za afya, huku zaidi ya watu 4,500 wakihudumiwa katika siku ya pili, Jumanne, Julai 14. Hivyo, idadi ya jumla ya wananchi waliopata huduma katika siku mbili za mwanzo imefikia zaidi ya 8,000.
Huduma walizopata ni pamoja na vipimo mbalimbali vya afya, kuonana na madaktari bingwa, ushauri wa kitaalamu, matibabu na kupatiwa dawa kulingana na maelekezo ya madaktari.
Hadi habari hii inakwenda mitamboni, zaidi ya watu 50 walikuwa wamejitokeza kuchangia damu katika banda la Mpango wa Taifa wa Damu Salama.
Baadhi ya wagonjwa waliobainika kuwa na matatizo makubwa au kuhitaji uchunguzi wa kina walipewa huduma za awali na kupelekwa katika hospitali mbalimbali kwa kutumia magari ya wagonjwa ili kuendelea na matibabu.
Akizungumza katika kambi hiyo, Makonda alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wizara ya Afya, madaktari, wakuu wa taasisi za afya pamoja na sekta binafsi kwa kuwezesha huduma za kibingwa kuwafikia wananchi wa Arusha na maeneo ya jirani.
“Ninawashukuru sana madaktari, wakuu wa taasisi zote pamoja na Wizara ya Afya kwa namna ambavyo wameendelea kuwaheshimu na kuwajali wananchi wa Arusha. Kila tunapohitaji msaada, wamekuwa tayari kutushika mkono,” alisema Makonda.
Alisema mafanikio ya kambi hiyo yametokana na ushirikiano uliopo kati ya Serikali, viongozi wa wananchi, hospitali za rufaa na taasisi mbalimbali za afya.
“Ni ukweli usiopingika kwamba nisingeweza kupata mafanikio haya bila upendo wa Serikali yetu inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wake,” alisema.
Makonda alieleza kuwa wananchi wengi wanaofika kambini hawana uwezo wa kumudu gharama za vipimo na matibabu katika mazingira ya kawaida.
“Wapo wananchi ambao hawana uhakika wa mlo mmoja kwa siku. Wengine hawana ajira na wanaumwa. Wapo walioanza kufanya vipimo hospitalini, lakini fedha zao zikaishia kwenye vipimo vya awali kabla hawajakamilisha matibabu,” alisema.
Makonda alisema ingawa wananchi wanapata huduma bila malipo, taasisi, hospitali, madaktari na wadau wanaoshiriki wameingia gharama kubwa.
Alisema gharama hizo zinahusisha usafiri wa madaktari, vifaa vya uchunguzi, dawa, miwani, malazi, chakula na mahitaji mengine muhimu katika utoaji wa huduma.
“Huduma hizi ni bure kwa mwananchi, lakini si bure kwa wale walioziwezesha. Madaktari wamesafiri, vifaa vya kupimia vina gharama, dawa zina gharama na hata miwani inayotolewa imelipiwa,” alisema.
Aliwasihi wananchi wanaopewa dawa, miwani au maelekezo ya matibabu kuyafuata kikamilifu.
“Haitakuwa na maana mtu apewe dawa, azitumie kwa siku mbili na kuziacha kwa sababu tu ameanza kujisikia vizuri. Dawa hizo zimegharimiwa. Naomba kila mwananchi afuate masharti na maelekezo yote anayopewa na madaktari,” alisema.
Makonda aliwahimiza wafanyabiashara, wamachinga, waendesha bodaboda na bajaji, wafanyakazi na wananchi wengine kutenga muda kwa ajili ya kupima afya.
“Kufunga duka lako au kusimamisha biashara kwa muda na kuja kupima afya kunaweza kuwa na faida kubwa kuliko kuendelea na biashara bila kujua hali yako. Ugonjwa unapokuwa mkubwa unaweza kumaliza mtaji wako wote,” alisema.
Alisema huduma hizo zinapatikana kwa wananchi wote bila kujali eneo wanakotoka, dini, kabila, chama cha siasa au hali yao ya kiuchumi.










Social Plugin