Na Mwandishi wetu, Dar
Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue amesema maandamano ni haki ya msingi inayotambuliwa na Katiba ya Tanzania, sheria za nchi pamoja na makubaliano ya kikanda na kimataifa, akisisitiza kuwa yanapaswa kufanyika kwa kuzingatia sheria na bila kuathiri haki za watu wengine.
Sefue Ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na Mtandao wa Mwananchi Digital, akisema kwamba maandamano yanaangukia katika haki ya kujieleza akieleza kwamba maandamano yanayostahili kulindwa kisheria ni yale yanayotekelezwa kwa amani na kufuata masharti yaliyowekwa na sheria.
"Unajua maandamano ni haki ya msingi kwenye Katiba yetu, sheria yetu, makubaliano ya kikanda na kimataifa na maandamano yanaingia kwenye kundi la kujieleza. Tofauti ambayo inaonekana kwenye nchi zetu, watu wanashindwa kutofautisha maandamano yenye sifa ya kujieleza na maandamano ya vurugu," amesema Sefue.
Ameongeza kuwa uhuru wa mtu mmoja haupaswi kukiuka haki za wengine, akitolea mfano maandamano yanayosababisha biashara kufungwa au yanayohusisha vitisho kwa wananchi. "Ukisema mimi naandamana kwa namna ambayo duka langu lifungwe hayo si halali. Hata ukibeba jiwe kwa namna ambayo utamfanya mtu aogope hayo si halali," amesema.
Sefue pia amesisitiza umuhimu wa waandaaji wa maandamano kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kabla ya kuyafanya ili mamlaka ziweze kutoa ushauri kuhusu njia zitakazotumika na kuhakikisha usalama wa washiriki pamoja na wananchi wengine, akisema utaratibu huo unalenga kuwezesha matumizi ya haki ya kuandamana kwa njia inayozingatia sheria na kulinda maslahi ya jamii kwa ujumla.

Social Plugin