Serikali imedhamiria kubadilisha maisha ya wananchi vitongojini kupitia usambazaji wa umeme unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na wananchi wamehimizwa kuchangamkia kuunganishiwa umeme kwenye vitongoji vilivyofikiwa.
Hayo yamesemwa Julai 15, 2026 na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu wakati wa hafla ya kuwasha umeme katika Kitongoji cha Mwamlula katika Kijiji cha Mseko na Kitongoji cha Kipeke katika Kijiji cha Masagi Wilaya ya Iramba Mkoani Singida.
“Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo ameuwezesha Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuweza kutekeleza majukumu yake kisawasawa na anaendelea kuiwezesha ili kutimiza azma ya kuwafikishia maendeleo wananchi vijijini na vitongojini,” amesema Balozi Kingu.
Amesema mpango uliopo ni kufikisha umeme kwenye vitongoji vyote 64,359 ifikapo Mwaka 2030 na kwamba hadi sasa asilimia 62.4 ya vitongoji imefikiwa.
Amewasisitiza wananchi kuhakikisha wanatumia umeme kubadilisha maisha yao ya kila siku kama ilivyo azma ya Serikali kwa kuanzisha miradi na shughuli mbalimbali ya kiuchumi kwani umeme ni fursa ya kubadilisha maisha.
“Mnaweza kubadilisha maisha yenu ya kila siku mkaongeza mapato ya kiuchumi kutokana na kufikiwa na umeme kwani pia huduma zingine za kijamii zinazotegemea umeme zitaanzishwa na zingine kuendelezwa,” amesema.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mha. Thomas Mbaga katika hafla hiyo amesema Mkoa wa Singida una jumla ya vitongoji 2,289, kati ya hivyo vitongoji 1,196 sawa na asilimia 52.25 tayari vimeunganishwa na umeme, huku vitongoji 1,093 sawa na 47.75% bado havijafikiwa na huduma na kwamba utekelezaji wa miradi unaendelea.
Mha. Mbaga amewasisitiza wananchi kuhakikisha wanalinda na kutunza miundombinu kwani Serikali inatumia fedha nyingi kutekeleza miradi ya kusambaza umeme na huku akitolea mfano kwa Mkoa wa Singida pekee kuwa hadi sasa takriban shilingi bilioni 94.6 zimetumika kutekeleza miradi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa vitongoji vya Mwamlula na Kipeke wameishukuru Serikali kwa kuwafikishia umeme na wamebainisha namna ambavyo unakwenda kubadilisha maisha yao.
“Tumefurahi kufikishiwa umeme, tutajitahidi kuhakikisha tunautumia pia kujiongezea kipato mbali na kutuangazia wakati wa usiku,” amesema Lucia Constantine mkazi wa kitongoji cha Mwamlula






Social Plugin