Na Jackline Minja, WMJJWM - Kakonko
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amewataka wananchi wa Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma kuendelea kushirikiana na Maafisa Maendeleo ya Jamii, kusimamia na kuendeleza miradi ya kiuchumi inayotekelezwa katika maeneo yao ili kuongeza kipato, kuinua ustawi wa familia na maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Mahundi metoa rai hiyo Julai 15, 2026, wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo wilayani humo, ikiwemo shughuli za Kikundi cha Wanawake Ubihumwe Kata ya Gwarama, kikundi cha vijana Tuinuane na Shule ya Msingi Itumbike yenye kitengo cha watoto wenye mahitaji maalum.
Amekutana pia na kikundi cha watu wenye ulemavu Kakonko pamoja na kuzindua jengo la kivuli cha Soko la Kijiji cha Kanyonza.
Amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa makundi mbalimbali ya wananchi kupitia mikopo, mafunzo na miradi ya maendeleo, hivyo ni wajibu wa wananchi kuitunza na kuisimamia miradi hiyo ili iwe na tija ya kudumu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Aidha, amewataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wao wa malezi kwa kuwajenga watoto katika maadili mema na kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyoathiri watoto na wanawake katika jamii.
"Tupige kelele kukataa ukatili wa kijinsia na tuwalinde watoto wetu ili wakue katika mazingira salama yatakayowafanya kuwa raia wema na wenye mchango kwa Taifa," alisema Naibu Waziri Mahundi.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kakonko, Mbunge wa Jimbo hilo, Mhe. Allan Mvano amesema ataendelea kuwa sauti ya wananchi wake kwa kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha ahadi alizozitoa kwa wananchi zinaendelea kutekelezwa kwa kushirikiana na Serikali, wadau wa maendeleo na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, kuhakikisha kunapatikana matunda katika sekta mbalimbali ya elimu, uwezeshaji wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu pamoja na kuboresha miundombinu ya huduma za kijamii.





Social Plugin