Na Alex Sonna, Dodoma
Katika hatua mpya ya kuimarisha afya ya jamii na ulinzi wa mazingira, Serikali imezindua mwongozo mpya wa usafi wa mazingira utakaotoa dira ya kitaifa katika usimamizi wa taka ngumu na majitaka, sambamba na kuimarisha huduma jumuishi zinazolenga kufikia wananchi wote mijini na vijijini.
Uzinduzi huo umefanyika leo Julai 2, 2026 jijini Dodoma wakati wa Kongamano la Kitaifa la Usafi wa Mazingira lililowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya maji na mazingira, likilenga kuunganisha juhudi za kuboresha mifumo ya utoaji huduma na kupunguza athari za uchafuzi wa mazingira nchini.
Akizungumza katika kongamano hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Prof. Paramagamba Kabudi, amesema mwongozo huo mpya ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuhakikisha Tanzania inakuwa na mifumo thabiti ya usafi wa mazingira inayowafikia wananchi wote bila kuachwa nyuma.
Amesema usafi wa mazingira ni nguzo muhimu ya afya ya wananchi na kichocheo cha maendeleo ya taifa, akibainisha kuwa Serikali imejipanga kuimarisha utekelezaji wa sera, sheria na miongozo ili kuhakikisha miji na vijiji vinakuwa safi, salama na endelevu.
“Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na miji na vijiji safi, salama na vinavyopendeza. Hili linawezekana endapo wananchi watashiriki kikamilifu na kujenga utamaduni wa kulinda mazingira yao,” amesema Prof. Kabudi.
Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka kipaumbele katika ajenda ya mazingira na nishati safi, hatua inayolenga kuboresha afya ya wananchi na kupunguza uchafuzi wa mazingira.
“Rais Samia amekuwa kinara wa nishati safi duniani, na ni muhimu kuendeleza kasi hii kuhakikisha wananchi wote wanatumia nishati salama na rafiki kwa mazingira,” amesisitiza.
Prof. Kabudi pia amekemea tabia ya baadhi ya wananchi kutumia mitaro ya maji kama dampo la taka, akionya kuwa hali hiyo inachangia kuziba mifumo ya maji na kuongeza hatari ya mafuriko pamoja na magonjwa ya mlipuko.
Amesema uwekezaji katika usafi wa mazingira ni uwekezaji katika afya ya taifa, akihimiza ulinzi wa vyanzo vya maji na utekelezaji madhubuti wa sheria na miongozo ya mazingira.
Kwa upande wa sekta ya miundombinu ya kijamii, amesisitiza kuboreshwa kwa huduma za vyoo katika maeneo ya mikusanyiko kama masoko, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa maji ya kunawa mikono ili kudhibiti maambukizi ya magonjwa.
Changamoto nyingine alizozitaja ni ongezeko la makazi holela na athari za mabadiliko ya tabianchi, akipendekeza kuimarishwa kwa mipango miji na upimaji wa viwanja ili kudhibiti ujenzi usio rasmi.
Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Kunti Majala, ameipongeza EWURA kwa kuandaa kongamano hilo, akisema limeweka msingi muhimu wa maboresho ya usimamizi wa sekta ya mazingira nchini.
Amesema vifo vinavyotokana na athari za mazingira mara nyingi husababishwa na shughuli za binadamu, hivyo elimu kwa wananchi inapaswa kupewa kipaumbele ili kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika, hususan kwa watoto.
Naye Mkurugenzi wa Fedha wa EWURA, Stanley Mahembe, amesema kati ya mamlaka 84 za maji nchini, ni 24 pekee ndizo zina mpango wa kutibu majitaka na tope la kinyesi, hali inayoonyesha bado kuna pengo kubwa la utekelezaji.
Ameongeza kuwa uzinduzi wa mwongozo huo utasaidia kuimarisha ufuatiliaji na utekelezaji wa huduma za usafi wa mazingira nchini.
“EWURA itaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha huduma za utibuji wa majitaka zinaimarishwa ili kulinda afya za wananchi na mazingira,” amesema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri, amesema ongezeko la kasi ya watu mkoani Dodoma limeongeza uhitaji wa mifumo imara ya usafi wa mazingira, akisisitiza kuwa wilaya ipo tayari kutekeleza miongozo mipya iliyozinduliwa ili kuboresha hali ya mazingira.









Social Plugin