Na Stella Herman,Shinyanga
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Shinyanga imeadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake kwa kukutana na wadau mbalimbali ambao ni walipa kodi, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya mamlaka hiyo na jamii pamoja na kutambua mchango wa walipa kodi katika maendeleo ya taifa.
Maadhimisho hayo yamefanyika Mkoani Shinyanga kwa kuwakutanisha walipa kodi wafanyabiashara, wajasiriamali na wadau wengine ,huku yakilenga kuhamasisha utii wa hiari wa kulipa kodi na kuadhimisha miaka 30 ya TRA.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo MkKatibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, CP Salum Hamduni, alisema kodi ndiyo nguzo kuu ya maendeleo ya nchi kwani mapato yanayokusanywa na TRA yanawezesha Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi.
Alisema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa katika sekta za afya, elimu, maji, miundombinu na nishati kupitia mapato ya ndani, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi na mfanyabiashara kutimiza wajibu wake wa kulipa kodi kwa wakati na kwa usahihi.
"Kulipa kodi si adhabu bali ni wajibu wa kila mwananchi mwenye shughuli za kiuchumi. Tunapolipa kodi tunachangia moja kwa moja maendeleo ya taifa letu na kuboresha huduma zinazowagusa wananchi kila siku," alisema Hamduni.
Aidha, aliipongeza TRA kwa mafanikio iliyoyapata katika kipindi cha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, akieleza kuwa mamlaka hiyo imeendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato, kuongeza uwazi katika utoaji wa huduma na kurahisisha ulipaji wa kodi kupitia matumizi ya teknolojia.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga, Ramadhan Sengo, amesema maadhimisho ya miaka 30 ya TRA ni fursa muhimu ya kutafakari mafanikio yaliyopatikana, kusikiliza maoni ya walipa kodi na kuimarisha ushirikiano unaochochea ongezeko la mapato ya Serikali.
Amesema kwa kipindi chote cha miaka 30, TRA imeendelea kuboresha huduma kwa walipa kodi kwa kutumia mifumo ya kidijiti, kutoa elimu ya kodi na kuweka mazingira rafiki yanayowasaidia walipa kodi kutekeleza wajibu wao kwa urahisi zaidi.
Sengo alisema ushirikiano kati ya TRA na walipa kodi umechangia kuongezeka kwa ufanisi wa ukusanyaji wa mapato, huku akiwahimiza wafanyabiashara na wananchi kuendelea kuwa waaminifu katika kutekeleza majukumu yao ya kikodi.
"Maendeleo ya nchi yetu yanategemea mchango wa kila mlipa kodi. Tunaendelea kuboresha huduma zetu ili kuhakikisha walipa kodi wanapata huduma kwa wakati na katika mazingira yenye uwazi na weledi," amesema.
Walipa kodi kupokea elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kodi, hatua iliyolenga kuongeza uelewa wa sheria za kodi na kujenga uhusiano mzuri kati ya TRA na wadau wake.






Social Plugin