Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

PAN AFRICAN SPEECH AND DEBATE DIALOGUE YAJIVUNIA KUJENGA KIZAZI CHA VIONGOZI WA AFRIKA WENYE UWEZO WA KUJENGA HOJA



Na Bora M. Fadhili, Arusha.

Programu ya Pan African Speech and Debate Dialogue imeendelea kujidhihirisha kama jukwaa muhimu la kuwajengea vijana uwezo wa kufikiri kwa kina, kuwasilisha hoja kwa kujiamini na kutumia ushahidi katika mijadala, huku waandaaji wakisisitiza dhamira yao ya kuipanua ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi nchini.

Akizungumza Leo Julai 16,2026 Mwanzilishi wa programu hiyo na mwalimu wa Shule ya Sekondari Butimba mkoani Mwanza, Godlove Shami , amesema wazo la kuanzisha programu hiyo lilizaliwa baada ya kushiriki programu ya Fulbright Teaching Excellence and Achievement (TEA) nchini Marekani, ambako alijifunza umuhimu wa kuwajengea vijana uwezo wa kuzungumza hadharani, kufanya tafiti na kushiriki mijadala yenye mtazamo wa kimataifa.

Pia amesema kupitia programu hiyo, wanafunzi wanapata fursa ya kujifunza namna ya kujenga hoja zenye mantiki, kusikiliza na kuheshimu mitazamo tofauti pamoja na kujiandaa kuwa viongozi wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa upande wake, mshirika wa programu hiyo kutoka Marekani, Adam Thane , amesema ushirikiano huo ulianza mwaka 2022 baada ya makubaliano na Godlove ya kuanzisha programu hiyo, ambayo sasa imefikia msimu wake wa nne.

 Amesema lengo kuu la ushirikiano huo ni kuwasaidia vijana kuondokana na hofu ya kuzungumza mbele ya hadhara na kuwapa ujuzi wa mawasiliano unaohitajika katika elimu, ajira na nafasi mbalimbali za uongozi.

Aidha, amesisitiza kuwa uwezo wa kueleza mawazo kwa ufasaha na kujenga hoja zenye mantiki ni msingi muhimu wa kuandaa viongozi wa Afrika watakaoweza kushindana na kukabiliana na changamoto za dunia ya sasa.

Naye mwakilishi wa taasisi ya TELTA bi Agustina Mtui  amesema taasisi hiyo, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, imeandaa mkakati wa kuanzisha klabu za mijadala katika shule mbalimbali za mkoa huo ili kuwapa wanafunzi wengi zaidi fursa ya kukuza vipaji vyao katika mawasiliano, uongozi na kujenga hoja.

Pia ameeleza kuwa walimu kutoka shule 11 tayari wamepatiwa mafunzo ya kuwa walezi wa klabu hizo, hatua itakayosaidia kuhakikisha programu hiyo inaendelea kuwa endelevu hata baada ya mashindano kumalizika.

Hata hivyo katika programu hiyo, washiriki walijadili mada mbalimbali, ikiwemo faida na changamoto za Biashara Huria Afrika (AfCFTA).
 Waandaaji wamesema kupitia mijadala hiyo, wanafunzi wanajengewa uwezo wa kufanya tafiti, kutumia teknolojia za kisasa, kufikiri kwa kina, kushirikiana na wenzao pamoja na kuwa viongozi wenye kujiamini na wenye uwezo wa kufanya maamuzi sahihi katika karne ya 21.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com