Na mwandishi wetu,Mara
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema kuna watu wanaolipwa fedha nyingi kutoka nje ya nchi kwa lengo la kuwachochea vijana wa Tanzania kufanya vurugu na kushiriki katika vitendo vinavyohatarisha usalama wa nchi, akisisitiza kuwa Serikali haiwezi kuvumilia vitendo vinavyohatarisha maisha ya wananchi.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika leo Jumatano, Julai 1, 2026, katika Viwanja vya Sokoine, Mugumu, Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Dkt. Mwigulu amesema watu hao wanajinufaisha kifedha huku wakiwatumia vijana kama chombo cha kutekeleza vitendo vya vurugu.
"Wanayafanyia biashara maisha ya Watanzania, halafu mnataka tuwachekee?"
Waziri Mkuu amedai kuwa vyombo vya dola tayari vimewakamata baadhi ya watu wanaohusika na mtandao huo, ambapo kwa mujibu wa maelezo yake, baadhi yao walikiri kulipwa kati ya Sh. Milioni tatu hadi milioni tano kwa mwezi ili kuwahamasisha vijana kushiriki katika vurugu.
Akifafanua zaidi, Dkt. Mwigulu amesema: "Mwingine mkoa mmoja kule Kusini alikuwa anatengeneza vibomu vya asili analipwa milioni tano, ameambiwa akipeleka vijana wakafe yeye atalipwa milioni 500. Ninyi mnaunganaje na watu wanaotuwazia mabaya? Kataeni, kila kijana akatae, usifanyiwe biashara maisha yako."
Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu aliwataka vijana wa Tanzania kutokubali kutumiwa na watu wanaowashawishi kufanya vitendo vya uhalifu kwa manufaa ya wengine. Aliwasisitiza kuwa walinde amani, usalama na mshikamano wa taifa, akieleza kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vinavyohatarisha usalama wa nchi.

Social Plugin