Na Mwandishi wetu, Kigoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema amani na usalama ni msingi mkuu wa maendeleo ya Taifa, akiwataka wananchi kuendelea kulinda tunu hizo ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na mazingira bora ya ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii.
Rais Samia amesema hayo leo Jumatatu Julai 20, 2026 mkoani Kigoma wakati akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Tabora hadi Kigoma na uzinduzi wa meli nne za mizigo katika Bandari ya Kigoma.
Amesema Serikali itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya usafiri na usafirishaji, lakini mafanikio ya miradi hiyo yanategemea uwepo wa amani na usalama nchini.
“Swala la amani na usalama wa nchi yetu ni kipaumbele cha kwanza na hatupaswi kulipuuza hata kidogo. Tukivuruga amani na usalama wa nchi yetu, maendeleo hayatashamiri na hayatakuwa na maana,” amesema Rais Samia.
Amewataka wananchi wa Kigoma na Watanzania kwa ujumla kuwa na utamaduni wa kuweka usalama mbele, akisisitiza kuwa maendeleo yanahitaji mazingira yenye utulivu na mshikamano
Rais Samia pia amewataka wananchi kutokubali kushawishiwa au kutumiwa na watu wenye nia ya kuvuruga amani ya nchi, akieleza kuwa kulinda usalama ni jukumu la kila Mtanzania.
“Amani na usalama ni maendeleo, na maendeleo ni amani na usalama. Sote tuwe macho na tuepuke kuwa wasaliti na maadui wa nchi yetu,” amesema Rais Samia.
Ameongeza kuwa ulinzi wa amani na usalama utaendelea kuiwezesha Tanzania kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, kuvutia uwekezaji na kukuza uchumi kwa manufaa ya wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.



Social Plugin