Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad, akijaribu kuwasha gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) wakati wa makabidhiano rasmi ya gari hilo kwa ajili ya Kituo cha Afya Tinde, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad, akikata utepe kuashiria makabidhiano rasmi ya gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) kwa ajili ya Kituo cha Afya Tinde, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. Kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Dkt. Kalekwa Kasanga.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad, akikata utepe kuashiria makabidhiano rasmi ya gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) kwa ajili ya Kituo cha Afya Tinde, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. Kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Dkt. Kalekwa Kasanga.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad, akimkabidhi ufunguo wa gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Dkt. Kalekwa Kasanga, wakati wa makabidhiano rasmi ya gari hilo kwa ajili ya Kituo cha Afya Tinde.

Muonekano wa gari jipya la kubebea wagonjwa (Ambulance) lililotolewa na Serikali kwa ajili ya Kituo cha Afya Tinde, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, ambalo limekabidhiwa na Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad.
Muonekano wa gari jipya la kubebea wagonjwa (Ambulance) lililotolewa na Serikali kwa ajili ya Kituo cha Afya Tinde, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, ambalo limekabidhiwa na Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad, akijaribu kuwasha gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) wakati wa makabidhiano rasmi ya gari hilo kwa ajili ya Kituo cha Afya Tinde, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad, akizungumza na mmoja wa wakazi wa Tinde wakati wa shughuli za kukabidhi gari la kubebea wagonjwa (Ambulance).
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad, amesema ataendelea kusimama mstari wa mbele kusukuma maendeleo ya wananchi kupitia Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa uwakilishi bora hauhitaji mtu kuwa na fedha mfukoni bali uwezo wa kubeba na kutatua changamoto za wananchi.
Mhe. Azza ameyasema hayo leo Julai 18, 2026 wakati akikabidhi gari jipya la kubebea wagonjwa (Ambulance) lililotolewa na Serikali kwa ajili ya Kituo cha Afya Tinde katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. Gari hilo amelikabidhi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Dkt. Kalekwa Kasanga.
Akizungumza mbele ya wananchi na viongozi mbalimbali, Mbunge huyo amesema anaifahamu vizuri Tinde na changamoto zinazowakabili wananchi wake, hivyo ataendelea kuzifikisha katika mamlaka husika hadi zipatiwe ufumbuzi.
"Niliwaambia matatizo ya wananchi wa Tinde na Jimbo la Itwangi kwa ujumla nayafahamu, najua majukumu yangu. Kuwatekelezea maendeleo wananchi si lazima uwe na fedha mfukoni, bali uwe na uwezo wa kusimama na kubeba matatizo yao," amesema.
Amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupeleka miradi ya maendeleo katika Jimbo la Itwangi, akisema Serikali imeonyesha dhamira ya dhati ya kuboresha huduma za afya, maji, barabara, umeme na miundombinu mingine muhimu.
Akizungumzia ambulance hiyo, Mhe. Azza amesema ni matokeo ya juhudi za muda mrefu za kuwasilisha mahitaji ya wananchi bungeni, akieleza kuwa Kituo cha Afya Tinde kilikuwa kimekaa kwa takribani miaka mitano bila gari la wagonjwa baada ya ambulance ya awali kupata ajali iliyosababisha kifo cha dereva.
Amekumbusha kuwa hata alipokuwa Mbunge wa Viti Maalum aliomba magari ya wagonjwa kwa ajili ya Tinde na maeneo mengine na kuyakabidhi, lakini baada ya moja ya magari hayo kupata ajali wananchi walibaki bila huduma hiyo muhimu Tinde.
"Mimi sina fedha za kununua ambulance, lakini nina uwezo wa kusimama Bungeni na kushawishi ili wananchi wangu wapate huduma wanazostahili. Leo Serikali imesikia kilio cha wananchi wa Tinde na gari hili limepatikana," amesema.
Mbunge huyo amewataka viongozi wa halmashauri kuhakikisha ambulance hiyo inatunzwa vizuri, iwe na sehemu salama ya maegesho na itumike kwa kuzingatia taratibu, huku akisisitiza kuwa makundi yanayostahili kupata huduma bila malipo yazingatiwe kwa mujibu wa sera za Serikali.
Amesema Kituo cha Afya Tinde kinahudumia idadi kubwa ya wananchi, ambapo kwa mwezi hupokea wagonjwa wa nje kati ya 700 hadi 1,000 na kinahudumia wajawazito wanaojifungua kati ya 200 hadi 250, jambo linalodhihirisha umuhimu wa kupatikana kwa ambulance hiyo mpya.
Mhe. Azza amewapongeza madaktari, manesi na watumishi wote wa afya kwa kujitoa kuwahudumia wananchi licha ya changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Mbali na sekta ya afya, Mbunge huyo ameeleza kuwa Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo, ikiwemo ukarabati wa barabara ya Tinde–Usule iliyokuwa haipitiki kipindi cha masika baada ya kutolewa zaidi ya shilingi milioni 300 kwa ajili ya maboresho yake.
Amesema pia zahanati ya Nshinshinulu katika Kata ya Nsalala itaanza kutoa huduma mwezi ujao, huku zahanati ya Mwamkanga ikiwa imepauliwa kwa fedha za Mfuko wa Jimbo shilingi Milioni 15.
Katika sekta ya umeme amesema ndani ya miezi sita vijiji na vitongoji 58 vya Jimbo la Itwangi vitapatiwa huduma ya umeme, ikiwemo maeneo ya Kijiji cha Jomu.
Akizungumzia changamoto ya maji, amesema kati ya vijiji 58 vya jimbo hilo, vijiji 34 bado havina huduma ya maji, lakini Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali huku ikisubiri utekelezaji wa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria.
Amebainisha kuwa tayari ameomba shule za bweni zenye changamoto kubwa ya maji, ikiwemo Kituli Sekondari, Samuye na Igalamya, zichimbiwe visima, na kwamba mtambo wa kuchimba visima tayari umewasili jimbo kwa ajili ya kuanza kazi.
"Tunataka wanafunzi wetu waanze kupata maji shuleni, lakini maji hayo pia yawanufaishe wananchi wanaoishi jirani na shule hizo",amesema.
Mbunge huyo pia amewataka wananchi wa Tinde kuacha kujenga ovyo ili kutoa nafasi kwa barabara na miundombinu mingine ya maendeleo, huku akiitaka halmashauri kuharakisha upatikanaji wa soko la kisasa pamoja na kutafuta eneo jipya la dampo kutokana na ukuaji wa kasi wa mji wa Tinde.
Aidha, amesema wananchi wanaisubiri kwa hamu stendi mpya ya mabasi na kwamba, kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Halmashauri, kilichobaki ni kukamilisha ujenzi wa choo kabla ya kuanza kutumika rasmi.
Mbunge huyo pia amesema ataendelea kufuatilia na kusimamia utatuzi wa changamoto zinazolikabili Kituo cha Afya Tinde, ikiwemo upungufu wa watumishi wa afya, nyumba za watumishi, ukosefu wa jengo la X-Ray pamoja na mashine zake, akiahidi kuziwasilisha na kuzifuatilia kwa mamlaka husika hadi zipatiwe ufumbuzi.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Tinde, Evance Munisi, amesema kituo hicho kinatoa huduma kwa wananchi wengi lakini bado kinakabiliwa na changamoto za ukosefu wa uzio, wodi za kutosha, mashine ya X-Ray pamoja na nyumba za watumishi.
Ameishukuru Serikali kwa kukipatia kituo ambulance hiyo na kumpongeza Mhe. Azza kwa kuendelea kukipa kipaumbele kituo hicho.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Dkt. Kalekwa Kasanga, ameishukuru Ofisi ya Rais – TAMISEMI pamoja na Mbunge wa Jimbo la Itwangi kwa juhudi zake za kuwaletea wananchi maendeleo.
"Mhe. Azza Hillal ni mfuatiliaji. Anafuatilia jambo lake hadi mwisho na anafanyia kazi ahadi anazotoa. Wananchi hamkufanya makosa kwenye uchaguzi mkuu. Tutasimamia matumizi sahihi ya gari hili ili lidumu, na changamoto za Tinde tumezipokea, huku baadhi yake tayari tukizifanyia kazi ikiwemo ujenzi wa uzio," amesema.
Diwani wa Kata ya Tinde, Japhar Kanolo, amesema wananchi watahakikisha ambulance hiyo inatunzwa vizuri na kumpongeza Mbunge huyo kwa juhudi zake za kufuatilia maendeleo ya kata hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Edward Ngelela, amesema Mhe. Azza ameonyesha mfano wa uongozi unaoweka mbele maslahi ya wananchi.
"Anawakilisha shida za wananchi wa Itwangi, si mambo binafsi. Tuna mwakilishi mzuri, tumpe ushirikiano wa kutosha. Anashirikisha viongozi wenzake, anasikiliza ushauri na ameweza kufanya mambo makubwa ndani ya muda mfupi",amesema Ngelela.
Kabla ya makabidhiano ya ambulance hiyo, Mhe. Azza amezindua vituo vitatu vya waendesha bodaboda alivyovitengeneza katika Kata ya Tinde na kuwataka vijana kuendelea kulinda amani na kuepuka kushawishika kufanya vitendo vinavyoweza kuvuruga utulivu wa nchi.
Katika hafla hiyo, viongozi wa mila wa Tinde wamemtunuku Mbunge huyo jina la kimila "Balele", lenye maana ya "Mlezi", sambamba na kumkabidhi fimbo na vazi la kimila kama ishara ya heshima na kutambua mchango wake katika kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Itwangi.





























































Social Plugin