KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidia wa Polisi, Edith Swebe akiongea na waandishi wa Habari

‎‎Na Constantine Mathias -Bariadi


JESHI la Polisi Mkoani Simiyu linawashikiliwa watu wawili Kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya aliyekuwa Mhandisi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA), wilaya ya Busega Safiel Senzota (37).


‎Inadaiwa kuwa tukio hilo la kikatili lilitokea Mei 25, 2026 katika eneo la Mwanogi wilaya ya Busega Mkoani humo.


‎Akizungumza leo Juni 4, 2026 na Waandishi wa Habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidia wa Polisi, Edith Swebe amesema kuwa mara baada ya tukio hilo kuripotiwa, Jeshi la Polisi kilianza Uchunguzi wa kina uliofanikisha kukamatwa Kwa mtuhumiwa mmoja tarehe 1.6.2026 jijini Dar es Salaam alikokuwa amekimbilia baada ya kutekeleza uhalifu huo.


‎Kamanda Swebe ameeleza kuwa katika mahojiano ya awali, mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na mauaji hayo na kudai kutekeleza tukio hilo Kwa kushirikiana na Mwalimu wa shule ya Sekondari Chegeni, mwenye umri wa miaka 30 (jina limehifadhiwa) aliyekuwa na urafiki wa karibu na marehemu ambaye naye amekamatwa.


‎"Mara baada ya kutekeleza tukio hilo, mtuhumiwa aliondoka na baadhi ya Mali za marehemu,. zikiwemo kompyuta mpakato (laptop) moja aina ya HP, Simu ya mkononi aina ya Samsung, pamoja na kadi ya benki la CRDB ya Marehemu" amesema na kuongeza.


‎"Uchunguzi wa awali uliofanyika umebaini kuwa watuhumiwa hao walikuwa na tamaa ya kuwania mali kwani inadaiwa watuhumiwa hao walikuwa na taarifa kwamba marehemu alikuwa na fedha zilizokusudiwa kununua gari kwa ajili ya Mradi wake wa utengenezaji wa matofali".


‎Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu linatoa onyo kwa watu wachache wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu kwa lengo la kujipatia kipato kisicho halali kuacha mara moja, kwani Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao, huku Jeshi hilo likisisitiza kuwa uhalifu haulipi na kwamba wahalifu wataendelea kusakwa na kukamatwa popote walipo.