Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WADAU WA USTAWI WA WATOTO WATAKA WAZAZI KUSIMAMIA MALEZI YA WATOTO KUONDOKANA NA MMOMONYOKO WA MAADILI



Na Wellu Mtaki,Kikombo-Dodoma

Wadau wa ustawi wa watoto wameeleza kuwa mmomonyoko wa maadili na kuongezeka kwa ushawishi wa tabia hatarishi miongoni mwa watoto ni miongoni mwa changamoto zinazohitaji ushirikiano wa wazazi, walezi, walimu na jamii kwa ujumla ili kulinda mustakabali wa kizazi kijacho.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika katika Kituo cha Malezi ya Watoto Kikombo jijini Dodoma, Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Faithmary Lukindo, amesema watoto wanahitaji malezi yanayojengwa katika misingi ya maadili mema pamoja na kupewa nafasi ya kushiriki na kusikilizwa ili kuwajengea kujiamini na uwajibikaji.

Amesema watoto wengi hukumbana na changamoto zinazotokana na mazingira wanayokulia, hali inayoweza kuwafanya kuathiriwa na mienendo isiyofaa iwapo hawatapewa malezi na mwongozo sahihi.

“Mtoto anapopewa nafasi ya kutoa maoni yake na kusikilizwa, hujenga kujiamini na kujitambua. Hii ni hatua muhimu katika kumwezesha kufanya maamuzi sahihi na kuepuka ushawishi wa tabia hatarishi,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Jukwaa la Haki za Watoto Tanzania, Sylvia Ruambo, amesema jamii ina wajibu wa kuhakikisha watoto wote wanapata ulinzi, upendo na haki sawa bila kujali mazingira wanayotoka.

Naye Askofu wa Kanda ya ECM Bethel, Richard Mwalyego, amesema utoaji wa elimu ya stadi za maisha ni sehemu ya suluhisho la changamoto zinazowakabili watoto, akitolea mfano mradi wa saluni ulioanzishwa katika Kituo cha Malezi ya Watoto Kikombo kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujitegemea.





Amesema watoto wanapopewa ujuzi wa kujiajiri na kujitegemea huongeza matumaini ya maisha yao ya baadaye na kupunguza uwezekano wa kujiingiza katika vitendo visivyofaa.

Awali, Mkurugenzi wa Kituo cha Malezi ya Watoto Kikombo, Darius Kalijongo, amesema kituo hicho kinakabiliana na changamoto za kitabia kutokana na watoto wengi kutoka katika mazingira tofauti ya kijamii na kifamilia.

Amesema ili kuimarisha usalama na malezi, kituo kimeweka mifumo ya uangalizi ikiwemo kamera za usalama pamoja na kuendesha miradi ya uzalishaji inayosaidia kuboresha ustawi wa watoto.

Maadhimisho hayo yameibua wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za dini, wazazi na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha watoto wanapata malezi bora yatakayowawezesha kuwa raia wema na wenye mchango chanya kwa taifa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com