Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UZUSHI KANDO: MAREKANI HAINA MGOGORO NA SERIKALI YA TANZANIA, SENETI YATAKA MARIDHIANO TU ILI MAMBO YAENDE


BUNGE la Seneti la Marekani limetaka kuanzishwa kwa mchakato wa mazungumzo ya kutafuta maridhiano ya kisiasa nchini ili kuirejesha nchi katika njia ya demokrasia.

Pendekezo hilo limo katika Muswada wa Mapitio ya Uhusiano wa Uwili baina ya Tanzania na Marekani uliowasilishwa katika Bunge la Seneti la Marekani jana.

Muswada wa awali ulikuwa umefanyiwa marekebisho wiki iliyopita lakini muswada uliopitishwa jana ulikuwa na nyongeza ambayo haikuwapo awali ya kutaka mazungumzo ya maridhiano yaanze.

Fasili B (4) ya Kifungu cha Saba cha muswada huo kinasema; “Kuanza kwa mazungumzo ya maridhiano na viongozi wa upinzani ili kujenga mustakabali mwema kwa taifa baada ya matukio ya vurugu za Oktoba 29.”

Pamoja na mambo mengine, muswada huo uliopitishwa umependekeza serikali ya Tanzania kuchukua hatua ya kufanya mabadiliko ya sheria za uchaguzi ili chaguzi zijazo ziwe huru na haki.

Kuna mabadiliko makubwa katika uandishi wa muswada uliopitishwa kulinganisha na ule uliofanyiwa marekebisho na hata ule wa awali.

Kwa mfano, katika Fasili B (1) ya Kifungu cha Saba, muswada uliorekebishwa ulikuwa unaagiza kubadili sheria za uchaguzi lakini uliopitishwa unazungumzia kuchukuliwa kwa hatua za kubadili.

Katika lugha ya kibunge, mabadiliko yaliyofanyika katika muswada huo yanamaanisha kwamba Bunge la Marekani sasa limejikita kwenye kuhakikisha Tanzania inapita kwenye mchakato na hatua muhimu badala ya kuiagiza cha kufanya.

Kama ilivyokuwa katika muswada uliofanyiwa marekebisho, muswada uliowasilishwa kwenye Bunge la Seneti umeruhusu pia Marekani kuendelea na ushirikiano wake wa kijeshi na kiusalama na Tanzania na kuachana na mapendekezo ya muswada asilia uliotaka Marekani iache kushirikiana na Tanzania.

Muswada mpya umekazia suala la kuwawekea vikwazo viongozi wa Tanzania watakaokutwa na hatia ya ukiukwaji wa haki za binadamu lakini badala ya kuweka vikwazo maalumu, muswada umetaka sheria rahisi zaidi ya kimataifa ya ‘Magnitsky’ itumike kwa ajili hiyo.

Pamoja na hilo, muswada umempa nguvu rais kutumia mamlaka yake kuamua endapo vikwazo hivyo vitumike au la.

Maana yake ni kwamba, hata kama muswada huu ukapitishwa na wabunge wa Marekani, vikwazo havitawekwa mpaka rais wao atakapoamua.

Muswada huo uliwasilishwa kwa ushirikiano wa wabunge wawili; Jeanne Shaheen wa Chama cha Democrat na Ted Cruz wa Chama cha Republic na lengo lake kuu lilikuwa ni kuishawishi serikali ya Marekani kufanya mapitio ya uhusiano wake na Tanzania.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com