

Katika
jitihada za kusogeza huduma karibu kwa wananchi, Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) Mkoa wa Shinyanga imeanza rasmi kutoa huduma kupitia ofisi inayotembea, hatua inayolenga kupunguza changamoto
ya walipakodi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma .
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo
katika mnada wa Tinde Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga leo Juni 16,2026 Afisa wa Kodi wa TRA
Mkoa wa Shinyanga Semeni Mbeshi amesema ofisi inayotembea imeanza rasmi
kutoa huduma katika eneo hilo ikiwa ni sehemu ya mkakati wa TRA wa kuwafikia
walipakodi moja kwa moja katika maeneo yao ya biashara.
Amesema huduma hiyo itawawezesha wananchi kupata
huduma mbalimbali za kikodi kwa urahisi, kupunguza gharama na muda wa kufuata
huduma katika ofisi za TRA pamoja na kutoa fursa ya kusikiliza kero zao na
kuzipatia ufumbuzi kwa wakati.
Kupitia ofisi inayotembea wananchi wamepatiwa
huduma zote zinazotolewa na TRA huku akitoa rai kwa wengine kuchangamkia fursa
hiyo .
Baadhi
ya wafanyabiashara waliohudumiwa katika mnada wa Tinde wameipongeza TRA kwa
kuanzisha huduma hiyo, wamesema imewarahisishia upatikanaji wa huduma na
kuwapunguzia usumbufu wa kusafiri umbali mrefu.
Wameiomba TRA kuendelea kupeleka huduma ya
ofisi inayotembea katika maeneo mengine ili walipakodi wengi zaidi wanufaike na
huduma hiyo, wakieleza kuwa hatua hiyo itachangia kuongeza ufanisi wa utoaji wa
huduma na kuimarisha ushirikiano kati ya mamlaka hiyo na wananchi.
TRA inaendelea kutoa huduma katika maeneo
mbalimbali kupitia ofisi inayotembea na kuwaomba kuchangamkia fursa hiyo.




Social Plugin