Kamanda wa kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoa wa Ruvuma Hamza Mwenda akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo (aliesimama pichani)Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Ruvuma imewasilisha tathmini ya utekelezaji wa programu za miradi ya maendeleo mkoani humo kwa lengo la kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kama ilivyokusudiwa bila kuwepo kwa vitendo vya rushwa.
Kikao hicho kilifunguliwa rasmi na mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka wilaya zote za mkoa.
Akiwasilisha taarifa hiyo katika ukumbi wa manispaa ya Songea juni 30, 2026, kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Ruvuma, Hamza Mwenda, amesema kuwa jumla ya miradi 290 ilifuatiliwa ambapo miradi 102 haikuwa na viashiria vya rushwa huku miradi 188 ikibainika kuwa na viashiria vya rushwa (red flag).
Kati ya miradi hiyo, miradi 43 ilifanyiwa uchunguzi na kusababisha kufunguliwa kwa kesi 20 mahakamani.
Kamanda Mwenda ameeleza kuwa maelekezo ya marekebisho yaliyotolewa kwa miradi yote 188 yenye viashiria vya rushwa yalifanyiwa kazi na wahusika.
Aidha, wadau wote wa miradi hiyo walijengewa uwezo kuhusu usimamizi wa miradi na mapambano dhidi ya rushwa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329 na marejeo yake ya mwaka 2023.
Amebainisha kuwa TAKUKURU hutekeleza jukumu hilo kupitia tafiti, uchambuzi wa mifumo, tathmini ya hatari ya rushwa pamoja na ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma.
Kwa mujibu wa kamanda Mwenda, baadhi ya changamoto zilizobainika ni pamoja na usanifu hafifu wa miradi, ongezeko la gharama za ujenzi, utekelezaji wa miradi chini ya viwango, ukiukwaji wa taratibu za manunuzi, kutokuwepo kwa mikataba, pamoja na ununuzi wa vifaa hewa.
Amewataka wananchi na wasimamizi wa miradi kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa rasilimali za umma kwa kuzingatia sheria, taratibu na kutoa taarifa pale wanapobaini viashiria vya rushwa.


Social Plugin