Na Shaban Juma, Dodoma
Naibu Waziri wa Afya, Dkt Florence Samizi amesema Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa vifaa tiba na rasilimali watu katika sekta ya afya ili kuongeza ufanisi wa huduma kwa wananchi, hususan watakaonufaika na huduma za Bima ya Afya nchini.
Dkt. Samizi ameyasema hayo leo Juni 19, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe Mohamed Mchengerwa kuhusu mkakati wa Serikali wa kuboresha vifaa tiba na rasilimali watu ili kuongeza ubora wa huduma za afya kwa wananchi, hususan katika maeneo ya vijijini.
Amesema katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2026, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa zaidi ya shilingi trilioni 1.2 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya afya pamoja na ununuzi wa vifaa na vifaa tiba katika ngazi zote za utoaji huduma kuanzia Hospitali ya Taifa, Hospitali za Rufaa za Kanda na Mikoa, Hospitali za Halmashauri, Vituo vya Afya hadi Zahanati.
Dkt. Samizi amesema kupitia uwekezaji huo, zaidi ya asilimia 85 ya vituo vya afya na zahanati nchini zimeboreshwa na kupatiwa vifaa muhimu vya uchunguzi na matibabu, huku hospitali za rufaa zikipatiwa vifaa vya kisasa ikiwemo mashine za CT-Scan, MRI na vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa maabara.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kuimarisha rasilimali watu katika sekta ya afya kwa kutekeleza ajira mpya za watumishi wa afya ili kuhakikisha huduma bora zinapatikana kwa wananchi katika ngazi zote za utoaji huduma.
Ameeleza kuwa katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, Serikali imeajiri jumla ya watumishi 5,000 wa kada mbalimbali za afya ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, hatua iliyoongeza idadi ya watumishi wa sekta ya afya kufikia 182,430 nchini.
Kwa mujibu wa Dkt. Samizi, kati ya watumishi hao, 142,794 sawa na asilimia 78 wanafanya kazi katika ngazi ya afya ya msingi, huku watumishi 34,047 sawa na asilimia 19 wakihudumu katika hospitali za rufaa za mikoa, kanda, maalum na taifa.
Amesema hatua hizo zinaendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi mijini na vijijini, sambamba na maandalizi ya utekelezaji wa mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote unaolenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya zenye ubora na kwa wakati.

Social Plugin