Na Jackline Minja, WMJWM- Dodoma
Serikali imeendelea kuimarisha mfumo wa usimamizi wa mikopo yenye masharti nafuu inayotolewa kwa wafanyabiashara ndogondogo ili kuhakikisha fedha hizo zinawanufaisha walengwa na kudhibiti upotevu wa fedha za umma.
Kauli hiyo imetolewa Juni 18, 2026 bungeni na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Tamima Haji Abass, aliyehoji kuhusu uwepo wa mwongozo na utaratibu wa kusimamia mikopo hiyo.
Mhe. Mahundi amebainisha kwamba, Serikali imeingia makubaliano na Benki ya NMB kusimamia utoaji wa mikopo yenye riba nafuu ya asilimia saba kwa mwaka kwa wafanyabiashara ndogondogo wanaokidhi vigezo vilivyowekwa, ikiwemo kuwa na kitambulisho cha kidijitali.
Amefafanua kuwa kabla ya mkopo kutolewa, biashara husika hutembelewa na kutathminiwa ili kujiridhisha kama inakidhi masharti ya kupata mkopo. Baada ya hapo, waombaji hupatiwa mafunzo ya usimamizi wa fedha na biashara kabla ya kupokea mkopo, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa matumizi ya fedha hizo na kuimarisha uwezo wa kurejesha mikopo kwa wakati.
“Marejesho ya mikopo hiyo yanafuatiliwa na maafisa wa Benki ya NMB kwa karibu ili kuhakikisha fedha za Serikali zinaendelea kuzunguka na kuwafikia walengwa wengi zaidi. Mfumo huo umewekwa mahsusi kuimarisha uwajibikaji na kupunguza changamoto za ucheleweshaji au kutorejeshwa kwa mikopo" amesema Mhe. Mahundi
Aidha, amesema utaratibu huo umeainishwa katika Mwongozo wa Utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa Wafanyabiashara ndogondogo kupitia Taasisi za Fedha wa mwaka 2024, ambao umeweka misingi ya utoaji na usimamizi wa mikopo hiyo nchini. Mwongozo huo unalenga kujenga mfumo endelevu wa uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia sekta ya biashara ndogo ndogo.
Hatua hizo zinaendelea kuonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo nafuu huku ikiimarisha mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji wa fedha za umma ili ziweze kuleta matokeo chanya kwa walengwa na maendeleo ya uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Social Plugin