Na Antonia Mbwambo- Mbeya
Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa Watumishi wa Umma kupitia utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa nyumba za makazi, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Patrick Allute, wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa nyumba za watumishi katika Shule za Msingi Ngolela, Wilaya ya Kyela na Idweli, Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya, iliyohusisha wataalamu kutoka Ofisi hiyo pamoja na Watumishi Housing Investments (WHI).
Bw. Allute amesema makazi bora yataongeza ari ya kazi kwa Walimu na kuboresha utoaji wa huduma. Aidha, amewataka Watumishi watakaonufaika na nyumba hizo kuzitunza vizuri mara zitakapokamilika kwa kuwa ni mali za umma na zinazopaswa kudumu ili kuwanufaisha Watumishi wa baadae.
"Serikali inaendelea kuwekeza fedha nyingi katika kuboresha mazingira ya kazi kwa Watumishi wa Umma, hivyo ni wajibu wa kila mnufaika kuhakikisha nyumba hizi zinatunzwa vizuri mara zitakapokamilika na kuanza kutumika ili ziendelee kuhudumia watumishi wa sasa na wa baadae," Bw. Allute amesema
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Mipango na Bajeti, kutoka Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Julieth Magambo, amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika ujenzi wa nyumba za watumishi ili kuhakikisha wanapata mazingira bora, salama na yenye utulivu yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Awali, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ngolela, Bw. Samsoni Anyosisye, ameishukuru Serikali kwa mradi huo, huku akieleza kuwa nyumba zilizopo zimechakaa na hazifai kwa matumizi, hali iliyowalazimu Walimu wengi kuishi mbali na shule.
Naye Mwalimu wa Shule ya Msingi Idweli, Bw. Tejile Mathew, amesema kukamilika kwa nyumba hizo kutaleta motisha ya kazi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma ya Elimu.




Social Plugin