Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AMANI YASISITIZWA, VIJANA WAKITAKIWA KUTUMIA FURSA ZA KIUCHUMI ZILIZOPO




Na mwandishi wetu, Dar

Wito wa kuendelea kulinda amani nchini umetolewa kwa vijana huku wakitakiwa kujiepusha na maandamano yenye uwezekano wa kusababisha vurugu na kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi.

Wakizungumza jijini Dar es Salaam, baadhi ya wananchi wamesema amani ndiyo msingi wa maendeleo na kwamba kila kijana ana wajibu wa kushiriki katika kuitunza kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Mkazi wa Kigogo, Dar es Salaam, Mtalemwa Simon, amesema endapo maandamano yataambatana na vurugu, athari zake zitakuwa kubwa kwa wananchi na taifa kwa ujumla, akisema shughuli za kijamii na kiuchumi zinaweza kusimama, bei za bidhaa mbalimbali kupanda kutokana na kuvurugika kwa usafirishaji na biashara, huku miundombinu ikipata uharibifu utakaoligharimu taifa fedha nyingi kwa ajili ya ukarabati.

“Tulinde amani kwani ndiyo msingi wa maendeleo. Vijana tuilinde amani ya nchi yetu,” amesema.

Kwa upande wake, Kamugisha Daniel, mkazi wa Dar es Salaam, amewataka vijana kutoshiriki maandamano yanayoweza kuleta hasara kwa wananchi na taifa, akitanabaisha kuwa hasara zinazotokana na vurugu huwarudia wananchi nyuma, hivyo vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wenzao kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa nchi.

Naye Mohamed Maliki, mkazi wa Kigogo, amesema vijana wanapaswa kujiepusha na kufuata mikumbo au makundi yanayoweza kuwashawishi kushiriki katika vitendo vinavyokiuka sheria. Amesisitiza kuwa badala yake wanapaswa kutumia fursa mbalimbali za elimu, ajira, biashara na ujasiriamali ambazo huendelea kupatikana katika mazingira yenye amani na utulivu.

Kwa nyakati tofauti, viongozi wa Serikali, viongozi wa dini, wazee wa kimila pamoja na makundi mbalimbali ya kijamii wameendelea kutoa wito wa kudumisha amani, wakisisitiza umuhimu wa kutatua tofauti kwa njia za kisheria na mazungumzo. Wito huo pia unakumbusha athari zilizoshuhudiwa wakati wa vurugu za Oktoba 2025, ambapo maeneo mbalimbali yaliathirika kwa kusimama kwa shughuli za kiuchumi na kijamii, baadhi ya miundombinu kuharibika na wananchi kupata hasara za mali, hali iliyodhihirisha umuhimu wa kuendelea kulinda amani na utulivu wa taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com