Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

POLISI WAFICHUA MPANGO WA UHALIFU JULAI 7

Jeshi la Polisi limetoa onyo kali kwa watu wote wanaohamasisha na kupanga kutekeleza vitendo vya uvunjifu wa amani na uhalifu nchini, wakiwemo wale wanaochochea kufanyika kwa maandamano mnamo tarehe 7 Julai mwaka huu.
Onyo hilo limetolewa kufuatia kuwepo kwa maswali mengi kutoka kwa baadhi ya wananchi hivi karibuni, wakitaka kujua jinsi jeshi hilo linavyofuatilia na kushughulikia uhamasishaji huo wa uvunjifu wa amani unaoendelea kufanywa na baadhi ya watu kupitia majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii.

Kupitia taarifa yake, Jeshi la Polisi limesema linafuatilia kwa karibu sana shughuli hizo zote kupitia mifumo yake mbalimbali pamoja na mitandao ya kijamii, ambapo imegundulika kuwa watu hao wameacha ajenda ya awali ya maandamano yasiyozingatia sheria na sasa wanahamasishana kufanya vitendo vizito vya kihalifu.

Miongoni mwa vitendo vya hatari vinavyohamasishwa ni pamoja na kufunga barabara, kuchoma moto shule kwa lengo la kusababisha taharuki kwa wazazi na walezi, kushambulia wananchi, kukata watu vichwa na kuua, pamoja na kuharibu mali za umma na za binafsi.

Aidha, watu hao wamediriki kwenda mbali zaidi kwa kuchocheana kupitia mitandao hiyo kuvamia askari wa vyombo vya ulinzi na usalama ili kuwapora silaha kwa ajili ya kwenda kuzitumia kutekeleza uhalifu wanaoupanga.

Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa uhamasishaji huo wa jinai unaofanyika chini ya kivuli cha kile wanachokiita haki ya kufanya maandamano ya amani haukubaliki hata kidogo, kwani ni kinyume kabisa na sheria za nchi, misingi ya utawala wa sheria, mikataba ya kikanda na kimataifa, na unahatarisha usalama wa Taifa.

Jeshi hilo limefafanua kuwa hakuna haki yoyote inayomruhusu mtu kuhamasisha uhalifu unaokusudia kuhatarisha usalama wa maisha ya watu na mali zao, au unaokiuka haki za wengine kwa kuwajengea hofu kila siku na kuwanyima uhuru wao wa kufanya shughuli zao za kila siku za kujitafutia kipato.

Kwa sababu hiyo, Jeshi hilo limesema hatua stahiki za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi ya wahusika wote, na jeshi linaendelea kuwafuatilia kwa karibu sana kwa mujibu wa sheria za nchi.

Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi wote nchini kuungana kwa pamoja katika kushirikiana kukataa na kupinga kwa nguvu zote vitendo hivyo vya kihalifu vinavyolenga kuhatarisha maisha ya wananchi, mali zao, mali za umma, pamoja na amani ya nchi.

Vilevile, limetoa ushauri kwa mtu yeyote anayepokea ujumbe unaohamasisha uhalifu wa aina hiyo kutousambaza kabisa, bali kuufuta mara moja na kutoa taarifa kwa vyombo husika ili hatua zichukuliwe.

Jeshi limewahakikishia wananchi wote kuwa hali ya usalama nchini itaendelea kuwa shwari, yenye amani, utulivu na usalama kamili, kwani mambo hayo yatalindwa na kudumishwa kwa ushirikiano wa karibu sana kati ya Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vyote vya ulinzi na usalama.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com