
Na Mbuke Shilagi Kagera
Mstahiki Meya wa Manispaa, Acton Jason Rwankomezi, leo Juni 11, 2026, amekutana na kuzungumza na wafanyabiashara wa Kata ya Rwamishenye ambapo amesikiliza na kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili katika eneo hilo.
Akizungumza katika mkutano huo, Rwankomezi amesema kuwa moja ya maelekezo ya Rais wa nchi Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kusikiliza wananchi na kutatua kero zao.
Amesema kuwa katika utekelezaji wa maelekezo hayo, amewasikiliza wafanyabiashara wa Rwamishenye, hususani wale wanaofanya biashara nje ya soko na barabarani, hali ambayo imekuwa ikiwanyima wateja wafanyabiashara waliopo ndani ya soko.
Kwa upande wake, Vivian Kakenk, muuzaji wa jumla wa nyanya anayefanyia biashara eneo la barabarani, amesema kuwa wafanyabiashara hao walihamishwa kutokana na ufinyu wa nafasi ndani ya soko.
Amesema walikubaliana kwa pamoja kuruhusu magari yasiyozidi mawili kushusha mizigo na kuepuka kupaki barabarani, lakini baadaye walielekezwa kurejea ndani ya soko ambapo ameomba mamlaka husika kuzingatia changamoto ya nafasi ndogo iliyopo sokoni na kuwaruhusu kuendelea kufanya biashara kwa utaratibu.
Wafanyabiashara wa samaki na dagaa waliopo ndani ya soko pia wameiomba Serikali kuhakikisha wafanyabiashara wanaofanya biashara nje ya soko wanaingizwa ndani ili kuwe na usawa wa kibiashara na kuongeza fursa za mauzo kwa wote.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Rwamishenye, Victor Baruani, amesema kuwa kutokana na ongezeko kubwa la wafanyabiashara wanaouzia nje ya soko, inaonekana wazi kuwa soko lililopo kwa sasa halitoshelezi mahitaji.
Ameshauri wafanyabiashara wote waelekezwe katika eneo ambalo tayari limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa soko jipya.
Naye Diwani wa Kata ya Rwamishenye, Mheshimiwa Sued Kagasheki, amewataka wananchi kuwa na subira wakati mamlaka husika zikifanya tathimini na kuweka utaratibu bora zaidi.
Amesema mahitaji ya huduma za soko yameongezeka kwa kiasi kikubwa huku soko lililopo likibaki dogo kulinganisha na idadi ya wafanyabiashara.
Akihitimisha mkutano huo, Mstahiki meya amesema kuwa mapendekezo na maoni yote yaliyotolewa na viongozi pamoja na wafanyabiashara yamepokelewa na yatafanyiwa kazi.
Amesema baada ya siku chache majibu rasmi yatatolewa ili kubaini hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa manufaa ya wafanyabiashara wote wa ndani na nje ya soko.















Social Plugin