Na mwandishi wetu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ameongoza kikao kazi cha mapitio ya mapendekezo ya marekebisho ya sheria mbalimbali zinazosimamiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya kiusalama na huduma kwa wananchi.
Katika kikao hicho, wajumbe walijadili mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi, Sura ya 322, Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168, pamoja na Kanuni za Ada za Usajili wa Shule za Udereva na Kanuni za Usalama Barabarani (Uthibitisho wa Bima za Magari) za mwaka 2026.
Aidha, kikao hicho kilijadili rasimu mbalimbali za mikataba na makubaliano ya ushirikiano wa kimataifa, ikiwemo Rasimu ya Mkataba kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Angola kuhusu masuala ya ulinzi wa raia, Rasimu ya Hati ya Makubaliano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Namibia katika masuala ya urekebu, pamoja na Rasimu ya Mkataba wa kuhamisha wafungwa kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mauritius.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Waziri Katambi alisisitiza umuhimu wa kufanya maboresho ya sheria na kanuni ili ziendane na mahitaji ya wakati na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za usalama na utekelezaji wa majukumu ya taasisi zilizo chini ya wizara.
Kikao hicho kimefanyika katika Ofisi Ndogo ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, jijini Dar es Salaam, na kimehusisha viongozi na wataalamu kutoka idara na taasisi mbalimbali zinazohusika na masuala yaliyojadiliwa.

Social Plugin