Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JMAT YAWATAHADHARISHA VIJANA KUEPUKA KUTUMIKA KUVURUGA AMANI KWA MASLAHI YA WATU WACHACHE

 

Mwenyekiti wa Jumuiya ya maridhiano na amani Mkoa wa Shinyanga (JMAT)Shehe Hamis Balilusa akizungumza kwenye mkutano wa jeshi la jadi sungusungu katika kata ya Jana wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga

Na  Stella Herman,Shinyanga

Vijana wametakiwa kujiepusha na vitendo vinavyochochea uvunjifu wa amani na kuacha kutumika  kwa maslahi ya watu wachache wanaolenga kuvuruga utulivu wa nchi badala yake wametakiwa kuwa walinzi wa amani, umoja na mshikamano pamoja na kukemea maovu katika jamii.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Mkoa wa Shinyanga (JMAT), Shehe Hamis Balilusa, wakati akizungumza katika mkutano wa Jeshi la Jadi Sungusungu uliofanyika  Kata ya Jana, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga

Shehe Balilusa amesema amani ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa, akisisitiza kuwa bila kuwepo kwa amani hakuna shughuli za kijamii wala za kiuchumi zinazoweza kufanyika kwa ufanisi.

"Vijana ni nguvu ya taifa msikubali kutumika kuvuruga amani ya nchi badala yake, simameni kuilinda, kuimarisha umoja na kushirikiana na vyombo vya dola katika kukemea vitendo vya uhalifu," amesema

Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Jadi Sungusungu Mkoa wa Shinyanga, John Kadama amewataka Sungusungu kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi ili kuhakikisha haki inatendeka na wananchi wanaendelea kuwa na imani na jeshi hilo.

Amesema viongozi wa zamani wa sungusungu wanapochanguliwa walikuwa wanakwenda kuangalia sungusungu inaendaje lakini viongozi wa sasa wanapochaguliwa wanaanza kutunisha mabega hawataki kujua misingi ya sungusungu,tunasema hakuna kujichukulia sheria mkononi zingatieni sheria za nchi na kusimamia ulinzi na amani inaendelea kutawala.

                 

Naye Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, amesema pamoja na mafanikio yanayopatikana katika kudhibiti uhalifu, bado mkoa huo unakabiliwa na changamoto za ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto pamoja na migogoro ya ardhi.

Amesema bado watoto wanafanyiwa ukatili wanabakwa,wanapigwa na kunyanyaswa pamoja na ukatili kwa wanawake ni mambo ambayo wanaendelea kuitaka Jamii iachane na vitendo hivyo huku akiwataka sungusungu kufuata sheria na taratibu ili kulinda amani na utulivu.

Kamanda Magomi ametoa rai kwa viongozi wa Sungusungu na wananchi kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi katika kutoa taarifa za uhalifu na kushughulikia migogoro kwa njia za kisheria, ili kuendelea kudumisha amani, usalama na utulivu katika jamii. 
         Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi 
             akitoa rai kwa sungusungu kuzingatia sheria za nchi   

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com