Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

EACOP YACHOCHEA AJIRA,UCHUMI NA MAENDELEO TANGA







Na Oscar Assenga, Tanga

WAZIRI wa Nishati, Dkt. Deogratius Ndejembi, amesema ujenzi wa Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) umefikia asilimia 86, huku mafuta ya kwanza yakitarajiwa kupokelewa katika Kituo cha Chongoleani, Tanga, na kusafirishwa Januari mwaka 2027.

Dkt. Ndejembi alisema hayo leo baada ya kutembelea eneo la mradi Chongoleani, mkoani Tanga, kujionea maendeleo ya utekelezaji wake, ambapo alieleza kuwa matarajio ni kukamilisha ujenzi huo ifikapo mwisho wa Agosti mwaka huu.

Alisema kazi nyingi muhimu zimekamilika na kilichobaki ni hatua za mwisho ikiwemo kukamilisha miundombinu ya umeme ili kuwezesha mitambo ya kusukuma mafuta kufanya kazi.

"Nimefurahishwa na maendeleo ya mradi. Kazi kubwa imefanyika na tunaamini ifikapo mwisho wa Agosti ujenzi utakuwa umekamilika. Ratiba inaonyesha kuwa meli ya kwanza itachukua mafuta ghafi kutoka Chongoleani mwezi Januari, 2027," alisema.

Hata hivyo, alisema changamoto iliyobaki ni kukamilika kwa njia ya umeme kutoka Majani Mapana kuelekea eneo la mradi, huku akiutaka mkandarasi anayetekeleza kazi hiyo chini ya Tanesco kuhakikisha anakamilisha mradi huo kwa wakati.

Alionya kuwa mkandarasi atakayeshindwa kutekeleza kazi hiyo ndani ya muda uliopangwa atachukuliwa hatua, ikiwemo kuondolewa katika orodha ya wakandarasi wanaofanya kazi na Tanesco.

Dkt. Ndejembi alisema EACOP ni mradi wa kimkakati kwa Tanzania, Uganda na ukanda mzima wa Afrika Mashariki, akibainisha kuwa bomba hilo lenye urefu wa zaidi ya kilomita 1,400 ni la kwanza duniani lenye mfumo wa kupashwa joto katika urefu wake wote.

Alisema Serikali ya Tanzania imewekeza zaidi ya Sh bilioni 973 kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), ambalo linamiliki asilimia 15 ya hisa za mradi huo kwa kushirikiana na kampuni za UNOC, TotalEnergies na CNOOC.

Aidha, aliwataka watanzania kuendelea kutumia fursa zinazotokana na mradi huo, akieleza kuwa zaidi ya Watanzania 3,000 wamepata ajira za moja kwa moja, huku vijana wengine zaidi ya 100 wakipelekwa Madimba kwa mafunzo ya kuongeza ujuzi kabla ya kuajiriwa.

Aliongeza kuwa zaidi ya vijana 400 kutoka Chongoleani wamepatiwa mafunzo na kuajiriwa katika maeneo mbalimbali ya mradi huo, huku fursa nyingine nyingi zikiendelea kujitokeza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, alisema mradi huo umeendelea kuleta manufaa makubwa kwa mkoa huo kupitia ongezeko la shughuli za Bandari ya Tanga, mapato ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na fursa za ajira kwa wananchi.

Alisema vifaa vingi vya mradi vimepitia Bandari ya Tanga kabla ya kusafirishwa katika maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa bomba hilo, jambo lililochochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.

Balozi Burian alisema pia mradi huo umezingatia viwango vya kimataifa vya utunzaji wa mazingira, akieleza kuwa shughuli za uvuvi zinaendelea kama kawaida na hakuna viumbe hai walioathirika kutokana na ujenzi wa gati na miundombinu mingine.

Aliongeza kuwa kupitia mradi huo, Halmashauri na jamii zinazozunguka eneo la mradi zimenufaika na miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa uwanja wa mpira unaotumiwa na klabu ya Coastal Union.

Naye Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Huduma za Mradi wa EACOP, Jofrey Mponda, ambaye pia alizungumza kwa niaba ya uongozi wa EACOP Tanzania, alisema mradi umefikia hatua za mwisho za utekelezaji, huku zaidi ya asilimia 90 ya kazi ikiwa imekamilika.

Alisema mradi huo unaounganisha mikoa 18 ya Tanzania na wilaya 27 umeingia katika hatua ya ukaguzi na makabidhiano ya mifumo mbalimbali, ikiwemo vituo vya kusukuma mafuta, matenki ya kuhifadhi mafuta na miundombinu mingine muhimu.

Mponda alisema pampu sita za kusukuma mafuta zimejengwa, mbili zikiwa nchini Uganda na nne nchini Tanzania, huku pampu mbili za kupunguza shinikizo la mafuta zikiwa Chongoleani.

Alibainisha kuwa matenki manne ya kupokelea mafuta tayari yamekamilika, huku kazi iliyobaki ikiwa ni kuunganisha mfumo wa umeme ili kuwezesha mitambo yote kuanza kufanya kazi kwa wakati.

Alisema EACOP inaendelea kushirikiana kwa karibu na Tanesco kuhakikisha miundombinu ya umeme inakamilika ifikapo Septemba mwaka huu, hatua itakayowezesha maandalizi ya kupokea mafuta ya kwanza mwezi Januari, 2027.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com