NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Serikali ya Ireland imesisitiza kuendelea kuunga mkono juhudi za kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake katika taasisi za elimu ya juu nchini Tanzania, ikieleza kuwa elimu jumuishi ni msingi wa maendeleo endelevu na jamii yenye usawa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa kitabu kinachohusu usawa wa kijinsia pamoja na mdahalo wa sera uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), jijini Dar es Salaam Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo katika Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania, Helen Counihan amesema uzinduzi wa kitabu hicho ni hatua muhimu katika safari ya muda mrefu ya kuimarisha usawa wa kijinsia ndani ya vyuo vikuu nchini.
Amesema kitabu hicho ni matokeo ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya Chuo cha Elimu cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUCE) na Trinity College Dublin (TCD), uliowezeshwa kupitia programu ya GATE ambayo imekuwa ikifadhiliwa na Ubalozi wa Ireland tangu mwaka 2018.
"Hii ni hatua muhimu inayodhihirisha mafanikio ya ushirikiano wetu katika kuendeleza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake ndani ya taasisi za elimu ya juu. Tunajivunia kuona matokeo ya programu ambayo tumekuwa tukiunga mkono kwa miaka kadhaa," amesema Counihan.
Amesema haki za wanawake na wasichana zinaendelea kuwa miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Ireland kupitia mkakati wake wa ushirikiano na Tanzania wa mwaka 2022–2026 pamoja na sera yake ya maendeleo ya kimataifa ya A Better World.
Counihan ameeleza kuwa maadili ya usawa wa kijinsia si ajenda ya Ireland pekee, bali ni sehemu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), akisisitiza kuwa wanawake na wanaume wanapaswa kupata fursa sawa za elimu bora bila ubaguzi.
Aidha, amesema Ireland itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania, asasi za kiraia, mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa maendeleo katika kuimarisha usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kupitia sekta ya elimu ya juu.
Amebainisha kuwa taasisi za elimu ya juu zina nafasi muhimu katika kuchambua na kubadili mitazamo na mila zinazochochea ukosefu wa usawa wa kijinsia, huku zikiendelea kuzalisha tafiti na ushahidi unaosaidia kutunga sera zenye kuzingatia mahitaji halisi ya jamii.
Counihan amesema programu ya GATE haikuwezesha tu uchapishaji wa kitabu hicho, bali pia imechangia kuzalishwa kwa tafiti na maarifa yatakayosaidia kupunguza pengo la usawa wa kijinsia katika sekta ya elimu.
Amesisitiza kuwa usawa wa kijinsia unapaswa kupewa kipaumbele, hususan katika taasisi za elimu ya juu ambako wanafunzi wana upevu wa kutosha wa kuelewa na kuutekeleza kwa manufaa ya jamii.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha DUCE, Profesa Amani Lusekelo, ameishukuru Trinity College Dublin kwa kuendelea kuongoza juhudi za kuimarisha usawa wa kijinsia chuoni hapo.
"Tutaendelea kushirikiana nanyi katika kufanya tafiti zaidi kuhusu usawa wa kijinsia ili kwa pamoja tuweze kunufaika na matokeo yake," amesema Prof. Lusekelo.




























Social Plugin