Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC MBONI MHITA AWEKA JIWE LA MSINGI JENGO LA KISASA LA BILIONI 5.3 USHETU, AMSIFIA CHEREHANI KWA KUSUKUMA MAENDELEO

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita (kulia), akiweka jiwe la msingi wa Jengo jipya la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu lililopo Nyamilangano, wilayani Kahama. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, akifungua mlango na kuingia rasmi ndani ya Jengo jipya la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu mara baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi huo wa kimkakati uliopo Nyamilangano.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mkoa wa Shinyanga, Stephano Gastory, akitoa maelezo kuhusu utekelezaji wa ujenzi wa Jengo jipya la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi iliyofanyika Nyamilangano.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, akiwa pamoja na Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani na viongozi mbalimbali wa Serikali, wakipanda lift ndani ya Jengo jipya la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, akitembelea na kukagua ukumbi wa mikutano ndani ya Jengo jipya la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu lililopo Nyamilangano, mara baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi huo
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, akiwa katika moja ya ofisi ndani ya Jengo jipya la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu wakati wa ziara ya kukagua mradi huo. Kulia kwake ameketi Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, huku kushoto akiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Gagi Lala.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita na Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, wakikata keki wakati wa uzinduzi na uwekaji wa jiwe la msingi wa Jengo jipya la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu lililopo Nyamilangano.
Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakigonganisha glasi (cheers) kuashiria mafanikio ya uzinduzi na uwekaji wa jiwe la msingi wa Jengo jipya la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu.
Muonekano wa Jengo jipya la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu lililopo Nyamilangano, wilayani Kahama, ambalo limejengwa kwa viwango vya kisasa kwa gharama ya zaidi ya Shilingi Bilioni 5.3.

Na Kadama Malunde - Ushetu, Shinyanga

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, leo Juni 16, 2026 ameweka jiwe la msingi la Jengo jipya la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu lililopo Nyamilangano, akisema mradi huo ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, iliyofanyika Juni 16,2026 Mhe. Mhita amesema Serikali ya Rais Samia imeendelea kuonyesha mapenzi makubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, maji, umeme, barabara na miundombinu ya utawala.
"Nimekuja kuweka jiwe la msingi katika jengo hili la kimkakati. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuonyesha mapenzi mema sisi wananchi wa Shinyanga. Tuna Rais mwenye maono na dhamira ya dhati ya kuboresha mazingira ya utoaji huduma na maeneo ya kufanyia kazi watumishi wa umma," amesema Mhita.

Ameeleza kuwa Mkoa wa Shinyanga umepokea zaidi ya Shilingi Trilioni 1.56 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha maisha ya wananchi.

Mhe. Mhita amesema jengo hilo lenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 5.3 litakapokamilika litatoa mazingira bora ya kazi kwa watumishi na kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.
"Jengo hili linatoa taswira ya Serikali inayojali watu wake. Linaboresha mazingira ya kazi, linaongeza ari ya utendaji na litawawezesha wananchi kupata huduma bora zaidi. Ukiingia katika jengo hili unajisikia fahari na faraja ya kufanya kazi katika mazingira ya kisasa," amesema.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wakandarasi wa kampuni ya Mzinga Holding Company Limited kuhakikisha wanakamilisha kazi zilizobaki kwa wakati ili ifikapo Agosti 8, 2026 jengo hilo liwe limekamilika na kuanza kutumika rasmi.

"Mkandarasi tumewaamini. Tunatarajia tarehe 8 Agosti 2026 tutakapokuja hapa tukute watumishi wapo ndani ya jengo hili wakitoa huduma kwa wananchi kwa kutumia mifumo ya kisasa," amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mhita amempongeza Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, kwa uongozi wake shirikishi na ushirikiano mzuri anaouonyesha katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), akishirikiana kwa karibu na Serikali, madiwani, watumishi wa halmashauri pamoja na viongozi wa chama katika kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.


TBA: Jengo la Kisasa Kukamilika Agosti 2026

Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mkoa wa Shinyanga, Stephano Gastory, amesema jengo hilo linajengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 5.39 na utekelezaji wake umefikia asilimia 93.
Meneja wa TBA Mkoa wa Shinyanga, Stephano Gastory

Amesema mradi huo unatekelezwa na Mzinga Holding Company Limited chini ya usimamizi wa TBA, huku ukitarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 8, 2026.

Kwa mujibu wa Gastory, jengo hilo la ghorofa lenye ukubwa wa mita za mraba 4,454.88 lina jumla ya ofisi 82, kumbi tatu za mikutano, vyumba saba vya kuhifadhia nyaraka, vyumba maalumu vya kuhifadhia mitihani na fedha, vyoo 41 pamoja na lift kwa ajili ya kurahisisha huduma kwa watumiaji wote wakiwemo watu wenye mahitaji maalumu.
Amesema mradi huo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM unaolenga kuimarisha mazingira ya kazi serikalini na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi. Pia umechangia kutoa ajira kwa wananchi wa Ushetu, kuongeza mapato ya Serikali kupitia kodi na kutumia bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi.

Cherehani: Mema Yaliyofanywa na Rais Samia Ushetu Hayawezi Kuelezeka kwa Siku Moja

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, amesema ujenzi wa jengo hilo ni tukio la kihistoria kwa wananchi wa Ushetu na ushahidi wa namna Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ilivyoleta mageuzi makubwa ya maendeleo katika eneo hilo.
Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani

"Hili ni tukio kubwa na la kihistoria kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu. Wengi wetu tulikuwa tunaota kuona maendeleo ya kiwango hiki, lakini leo tunashuhudia kwa macho yetu. Jengo hili la kisasa limejengwa katika eneo la Nyamilangano, zaidi ya kilomita 50 kutoka Manispaa ya Kahama, jambo linalodhihirisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kupeleka maendeleo hadi maeneo ya vijijini. Mhe. Mkuu wa Mkoa, naomba umfikishie Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan salamu za shukrani kutoka wananchi wa Ushetu. Mchango wake katika maendeleo ya jimbo letu ni mkubwa kiasi kwamba ni vigumu kuueleza kwa siku moja; tukiamua kuandika mafanikio haya kurasa zitaisha, na tukiamua kuyasimulia tunaweza kuzungumza hadi usiku bila kumaliza," amesema Cherehani.

Ameeleza kuwa pia Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza zaidi ya Shilingi Bilioni 5 kwa ajili ya ujenzi wake, jambo linaloonyesha dhamira ya kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi hata waliopo maeneo ya vijijini.

Mbunge huyo a,esema katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia, Jimbo la Ushetu limepokea zaidi ya Shilingi Bilioni 214 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Ametaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 3, uboreshaji wa huduma za afya kupitia vifaa tiba vya kisasa, pamoja na kuongezeka kwa watumishi ambapo mwaka huu pekee zaidi ya watumishi 136 wamepangiwa kufanya kazi Ushetu katika sekta za afya na elimu.
Pia amesema baada ya uchaguzi mkuu, Serikali imetoa zaidi ya Shilingi Bilioni 1.7 kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe na ujenzi wa madarasa mapya.

"Sisi wananchi wa Ushetu tunampenda sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Tunaendelea kumuombea na tutaendelea kushirikiana na Serikali yake katika kuwaletea wananchi maendeleo. Kazi yetu sisi viongozi ni kuwafikia wananchi, kusikiliza changamoto zao na kuzitatua kwa kushirikiana na Serikali," amesema Mhe. Cherehani.

Mbunge huyo pia amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Bi. Hadija Kabojela, kwa mchango wake mkubwa katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

"Mkurugenzi wetu Hadija Kabojela ni miongoni mwa watumishi wanaojituma sana. Anafanya kazi kwa bidii kubwa kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa wakati na wananchi wanapata huduma stahiki. Tunathamini mchango wake pamoja na watumishi wote wa halmashauri, madiwani na viongozi wa Chama cha Mapinduzi kwa ushirikiano wanaoutoa," amesema Mhe. Cherehani.

Kabojela: Jengo Litaongeza Ufanisi wa Huduma kwa Wananchi

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Bi. Hadija Kabojela, amesema kukamilika kwa jengo hilo kutaongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa kuwa idara zote muhimu za halmashauri zitapatikana eneo moja.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Bi. Hadija Kabojela

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuweka mazingira bora ya kazi kwa watumishi wa umma na kwamba Halmashauri ya Ushetu itaendelea kusimamia vyema rasilimali zinazotolewa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na zenye tija.

Kabojela amewashukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita, Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mhe. Emmanuel Cherehani, madiwani, viongozi wa CCM na wananchi kwa ushirikiano mkubwa unaowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Frank Nkinda, ampongeza Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, kwa kuendelea kusimamia maendeleo ya wananchi wake, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Hadija Kabojela, kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo.
Aidha, ameeleza kuwa jengo hilo la kisasa lenye huduma ya lift ni miongoni mwa majengo bora ya utawala katika Mkoa wa Shinyanga na ni matokeo ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha miundombinu ya utawala na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Gagi Lala, amesema maendeleo yanayoonekana katika halmashauri hiyo yanatokana na ushirikiano mkubwa wa viongozi wote na wananchi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Gagi Lala.

Amesema Serikali imeendelea kuleta fedha nyingi za maendeleo na kwamba halmashauri itaendelea kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa kwa manufaa ya wananchi wa Ushetu.

Nao baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo wamesema ujenzi wa jengo hilo la kisasa ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha miundombinu ya utawala na kusogeza huduma karibu na wananchi.

Wamesema mradi huo utaongeza ufanisi wa utoaji huduma katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu na ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayolenga kuharakisha maendeleo na kuboresha ustawi wa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.


Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com