Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Mgogoro unaohusu zaidi ya wafanyabiashara 300 wa Soko la Rehema Nchimbi umeibuka jijini Dodoma, baada ya kundi hilo kulalamikia kuzuiwa kuendelea na shughuli za biashara katika eneo mbadala la Umonga waliloelekezwa na Serikali, hali inayodaiwa kudumaza kipato chao kwa zaidi ya miezi saba sasa.
Wafanyabiashara hao wanadai walioondolewa katika eneo la awali Oktoba mwaka jana kufuatia hatua ya Bunge la Tanzania kuchukua eneo hilo, wanasema pamoja na jitihada za Serikali kuwatafutia eneo mbadala, utekelezaji wa maamuzi hayo umekuwa na changamoto kubwa katika ngazi ya uongozi wa jiji.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wenzake, Prisca Chibwaye amesema tangu kuondolewa katika vibanda vyao bila fidia, wamekuwa wakikosa mahali pa kuendeshea biashara licha ya kuoneshwa eneo la Umonga kama mbadala rasmi.
Ameeleza kuwa ziara ya Mwigulu Nchemba aliyoifanya mapema mwaka huu ilitoa matumaini baada ya kuagiza wafanyabiashara wote waliopisha eneo hilo kuhamishiwa Umonga, sambamba na maagizo ya kuboreshwa kwa miundombinu ikiwemo kumwaga kifusi ili kuzuia maji ya mvua.
Hata hivyo, amesema hadi sasa utekelezaji wa maagizo hayo haujakamilika, hali inayochochea sintofahamu kati ya wafanyabiashara na mamlaka za jiji.
“Ni zaidi ya miezi saba sasa hatujafanya biashara,tuna mikopo, familia zinatutegemea, lakini hatuna chanzo cha kipato,tunaiomba Serikali iingilie kati ili tupate suluhisho la haraka,” amesema.
Kwa mujibu wa wafanyabiashara hao, changamoto zinazowakabili katika eneo jipya ni pamoja na ukosefu wa miundombinu muhimu kama maji, umeme na vyoo, pamoja na ucheleweshaji wa uwekaji wa kifusi kilichoelekezwa. Wamedai kuwa kati ya magari 18 ya kifusi yaliyopangwa, kiasi kidogo tu ndicho kimewasilishwa.
Aidha, Katibu wa Bodi ya Wadhamini wa soko hilo, Abdullah Gogo, amesema kufungwa kwa soko hilo bila notisi ya kutosha kumeathiri ustawi wa kiuchumi wa wafanyabiashara wengi waliokuwa wakitegemea biashara hizo kama chanzo kikuu cha mapato.
Amebainisha kuwa wafanyabiashara hawapingi maamuzi ya Serikali wala ofisi ya Bunge, bali wanachokiona ni changamoto katika utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa juu ya matumizi ya eneo mbadala.
Katika upande mwingine, uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma umekanusha tuhuma za kuwazuia wafanyabiashara hao kwa makusudi, ukieleza kuwa ucheleweshaji uliopo unatokana na kutokamilika kwa taratibu za kisheria.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji, Nsubisi Kapura amesema tayari jiji lilishatoa mikataba kwa wafanyabiashara hao ili kurasimisha matumizi ya eneo hilo, lakini baadhi yao wamekataa kusaini, wakitaka kuanza biashara bila kulipia gharama za awali.
Aidha, ameeleza kuwa kuna hoja ya baadhi ya wafanyabiashara kutaka kuongeza idadi ya watu wasiokuwepo kwenye orodha rasmi, jambo ambalo linakinzana na utaratibu uliowekwa.
“Suala la mkataba ni la msingi kisheria. Eneo ni mali ya Serikali, hivyo haliwezi kutumika bila makubaliano rasmi. Hata maelekezo ya Serikali yamesisitiza umuhimu wa utaratibu huo,” amesisitiza.
Kutokana na mvutano huo, wadau mbalimbali wanaona umuhimu wa Serikali kuu kuingilia kati ili kuweka uwiano kati ya ulinzi wa taratibu za kisheria na uhai wa kiuchumi wa wafanyabiashara, ili kuepusha kuendelea kwa athari za kijamii na kiuchumi zinazoweza kujitokeza endapo suluhisho la haraka halitapatikana.




Social Plugin