Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TUJIKUMBUSHE MACHUNGU YA OKTOBA 29: KWANINI RIPOTI YA JAJI CHANDE NI DAWA YA KUDUMU YA KULINDA MAISHA YA WATANZANIA

Ujumbe wa Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman unapaswa kupokelewa kama msingi imara wa mustakabali wa nchi yetu, tukikumbuka madhila mazito yaliyowasibu wananchi kufuatia machafuko na fujo zilizotokea baada ya uchaguzi wa Oktoba 29. 

Tukio hilo liliacha kovu kubwa katika mioyo ya Watanzania wengi kutokana na kusimama kwa shughuli za kiuchumi na kijamii, ambapo wafanyabiashara walikosa wateja na sheli za mafuta zilifungwa, hali iliyosababisha usafiri kuwa wa shida na gharama za maisha kupanda ghafla. Hakuna Mtanzania anayetamani kurejea katika kipindi kile ambacho hata mahitaji ya msingi kama chakula yaligeuka kuwa anasa, huku bei za bidhaa kama mchele, unga, na nyanya zikipaa kiasi cha nyanya mbili tu kuuzwa hadi shilingi elfu moja, jambo lililoumiza familia nyingi mitaani kwetu.

Athari hizo hazikuishia kwenye uchumi pekee, bali zilivuruga kabisa mfumo wa huduma za kijamii na kuwanyima watoto wetu haki yao ya msingi ya kupata elimu ndani ya siku hizo za taharuki. 

Shule zilifungwa na mazingira ya kupata huduma za afya yakawa magumu, jambo linalothibitisha kuwa uvunjifu wa amani haubagui na badala yake unarudisha maendeleo ya taifa nyuma kwa miaka mingi. 

Kwa kuzingatia machungu hayo, ni wazi kuwa ushauri wa Jaji Chande wa kutaka tutumie mifumo yetu ya ndani kusuluhisha migogoro ni wa busara kubwa, kwani fujo hazileti katiba mpya wala tume huru, bali zinaleta umaskini, njaa, na uharibifu wa mali za wananchi wanyonge ambao wamejitafutia kwa jasho lao.

Hivyo basi, huu ni wito kwa vijana na wananchi wote kwa ujumla kukataa kutumika katika harakati zozote za uvunjifu wa amani ambazo mwisho wake ni hasara kwa taifa na maumivu kwa mtu mmoja mmoja. 

Tunapaswa kuwa macho na vishawishi vinavyoweza kutuingiza katika fujo zinazokusudiwa kurudisha nyuma ukuaji wa biashara na ustawi wa jamii yetu. 

Ni wajibu wetu sote kulinda utulivu tulionao kwa sababu bila amani hakuna biashara itakayostawi, hakuna mtoto atakayesoma, na gharama za maisha zitaendelea kuwa mzigo mkubwa kwa mwananchi wa kawaida. Tuungane kuienzi ripoti ya Jaji Chande kama dira ya kisheria na ya kizalendo ili kuhakikisha kuwa madhila ya Oktoba 29 hayajirudii tena katika ardhi ya Tanzania.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com