
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Mkoa wa Shinyanga, Sheikh Balilusa Khamis, ameiomba serikali kutozipuuza kauli zinazotolewa na baadhi ya watu, hususan viongozi wa kijamii na kisiasa, ambazo zinaweza kuhatarisha usalama wa wananchi na utulivu wa taifa, bali zichukuliwe hatua stahiki mapema ili kulinda amani ya nchi.
Akizungumza katika mahojiano maalum kuhusu kuimarisha mshikamano wa kijamii, amesema kuna mwenendo unaojitokeza wa baadhi ya watu kutoa maneno yasiyo na staha na yasiyo sahihi, jambo ambalo linaweza kuchochea taharuki na migogoro isiyo ya lazima endapo halitodhibitiwa mapema na hivyo kuhatarisha amani na utulivu wa taifa.
Amesema suala la amani si la kubezwa, bali ni jukumu la msingi la serikali na wananchi wote kuhakikisha linaendelea kudumu.
Ameonya kuwa mtu mmoja mwenye kauli potofu anaweza kusababisha madhara makubwa kwa jamii, akibainisha kuwa historia inaonesha migogoro mingi huanzia kwenye maneno yasiyopimwa.
“Ni muhimu watu wakakemewa mapema. Kauli zisizo na msingi zinaweza kuleta maafa makubwa. Serikali inapaswa kuwa makini na kuchukua hatua dhidi ya upotoshaji unaoendelea,” amesisitiza Sheikh Balilusa.
Amesema Tume ya kuchunguza matukio ya wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 imefanya kazi kubwa na inapaswa kuungwa mkono kwa kutekeleza mapendekezo yake ili kuimarisha uwajibikaji na amani nchini.
Kwa upande wa vijana, amewataka kutambua mabadiliko chanya yaliyopatikana nchini kwa kulinganisha maisha ya sasa na ya zamani.
Amesema vijana wanaolalamikia hali ya maisha wanapaswa kuwauliza wazee wao ili kuelewa safari ya maendeleo iliyopatikana ikilinganishwa na hapo awali.
Ameeleza kuwa tofauti na zamani ambapo huduma muhimu kama umeme na miundombinu bora zilikuwa adimu, kwa sasa kumekuwa na maboresho makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, makazi na huduma za kijamii.
Aidha, amekosoa tabia ya baadhi ya watu kulinganisha maisha ya Tanzania na nchi nyingine bila kuzingatia mazingira halisi ya kila taifa, akisema mtazamo huo unaweza kupotosha fikra za wananchi na kudhoofisha ari ya kujenga nchi yao.
“Tunapaswa kujivunia tulichonacho na kuendelea kukijenga. Kukimbilia kulinganisha na mataifa mengine bila uelewa ni hatari kwa ustawi wa taifa letu,” amesema.
Amebainisha kuwa katika baadhi ya nchi, migogoro imekuwa ikichochewa na kauli za wanasiasa wanaopotosha ukweli ili kujijengea umaarufu, hali ambayo amesema inaweza kujitokeza pia endapo jamii haitakuwa makini na uchambuzi wa taarifa wanazozipokea.
Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa jukumu la kulinda amani ni la kila Mtanzania, akiwataka wananchi kushirikiana na serikali katika kukemea vitendo na kauli zinazoweza kuvuruga utulivu wa nchi.
Social Plugin