Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SAUTI ZA KIROHO NA KISIASA KUHUSU MARIDHIANO KATIKA KUPONYA TAIFA

Viongozi wa dini nchini wameshauri mchakato wa kupata maridhiano ya kitaifa uwe shirikishi na uepuke maslahi binafsi ili kuliponya taifa kwa dhati. 

Askofu Msaidizi Mstaafu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Method Kilaini, ameshauri tume inayotarajiwa kuundwa iruhusu watu kuwa huru kutoa yaliyopo mioyoni mwao, akitolea mfano nchi za Afrika Kusini na Rwanda ambazo zilifanikiwa kuponya mataifa yao kupitia mazungumzo ya wazi licha ya kupitia migogoro mikubwa. 

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Alhad Mussa Salum, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kuunda Tume ya Maridhiano kufuatia ripoti ya matukio ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, akisisitiza kuwa maridhiano ya kweli yanahitaji watu kuwa wazalendo na kukubali kusamehe sehemu ya haki zao badala ya kila upande kuvuta kamba kwake. 

Mtazamo huo umeungwa mkono na Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Nuhu Mruma, aliyebainisha kuwa lengo kuu la tume hiyo linapaswa kuwa ni kuunganisha pande zinazotofautiana ili taifa lisonge mbele, huku akishauri mkazo mkubwa wa maridhiano uelekezwe kwa wanasiasa.

Hatua hii imekuja baada ya Rais Samia kutangaza uamuzi wa kuunda Tume ya Maridhiano kama sehemu ya kutekeleza mapendekezo ya kamati iliyochunguza matukio ya wakati na baada ya uchaguzi uliopita

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia kwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, kilieleza kuwa kinaamini maridhiano ni njia sahihi na endelevu ya kujenga taifa imara, huku kikisisitiza kuwa hatima ya nchi haiwezi kujengwa kwa misimamo mikali bali kwa uwezo wa pande zote kukaa pamoja na kusikilizana. 

Mwanasiasa mkongwe  Hamad Rashid Mohammed ameshauri kuwa mchakato wa maridhiano usijifungie kwa vyama vya siasa pekee, bali uhusishe makundi mapana ya kijamii yakiwemo asasi za kiraia, viongozi wa kimila, wazee, vijana, na vyombo vya habari ili kuepusha migongano ya kimaslahi wakati wa utekelezaji.

Wagombea urais wa zamani wa uchaguzi wa mwaka 2025 nao wamechangia mawazo yao wakitaka amani na utulivu vipewe kipaumbele cha kwanza kwa kufuata na kuheshimu sheria za nchi. 

Yustas Rwamugira wa TLP na David Mwaijojele wa CCK walishauri kuwa tume hiyo iongozwe kwa roho ya uvumilivu na ishirikishe pia wataalamu wa sheria pamoja na makundi maalum kama watu wenye ulemavu, wanawake, na wastaafu kwa kuwa changamoto zilizojitokeza ziligusa taifa zima. Wakati huohuo, Salum Rashid wa UDP alionya wajumbe watakaoteuliwa kujiepusha na uchochezi na kushauri serikali iwekeze nguvu na bajeti maalum kuwakusanya vijana kutoka mikoa iliyokumbwa na vurugu ili kuwapa nafasi ya kuridhiana.

Coaster Kibonde wa Chama cha Makini alihimiza tume hiyo ijiepushe na ubinafsi ili kupata suluhu ya pamoja inayogusa sekta zote za kijamii. Wasiwasi wa wanasiasa kutafuta madaraka pekee badala ya maslahi ya umma uliibuliwa na Kunje Ngombale Mwiru wa AAFP, aliyesisitiza kuwa maridhiano ya kweli yanapaswa kuleta tija ya muda mrefu katika huduma za kijamii, miundombinu, afya, na uwekezaji, na kwamba jambo hili linaweza tu kufanikiwa ikiwa litasimamiwa na watu wenye hofu ya Mungu na nia ya dhati ya kulinda mustakabali wa nchi. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com