Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA WA MAMA SAMIA WAANZA KUTEKELEZWA KISHAPU

Na Sumai Salum- Kishapu


Wananchi wilayani Kishapu mkoani Shinyanga wameaswa kujitokeza kwa wingi kunufaika na huduma ya msaada wa kisheria inayotolewa kupitia kampeni maalum iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ijulikanayo kwa jina la Kampeni ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia (MSLAC).



Akizungumza wakati akiipokea timu ya watalamu kuhusu zoezi hilo mei 6,2026, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Masindi, ameipongeza timu hiyo inayozunguka katika Kata zote 29 za Wilaya hiyo kwa lengo la kusogeza huduma za kisheria karibu na wananchi.


“Huduma hii ni muhimu sana kwa wananchi wetu, hususan wale wa kipato cha chini ambao mara nyingi wanashindwa kupata haki zao kutokana na gharama kubwa za mawakili. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuanzisha kampeni hii inayowafikia wananchi moja kwa moja,” amesema Mhe. Masindi.


Aidha, ameongeza kuwa upatikanaji wa haki ni msingi wa amani na maendeleo ya jamii.“Amani ni chanzo cha jamii kukua kiuchumi, kuwa na afya njema na familia imara,” amesisitiza.



Msajili Msaidizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Mratibu wa zoezi hilo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Abednego Madole, ameahidi kuwa timu yake itahakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi wote wa Kishapu.


“Tumejipanga kuhakikisha kila mwananchi anapata fursa ya kusikilizwa na kusaidiwa. Tutafika maeneo yote yaliyopangwa ili kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma,” amesema Madole.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi akizungumza wakati akiipokea timu ya watalamu kuhusu huduma ya msaada wa kisheria inayotolewa kupitia kampeni maalum iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mei 6,2026 ofisini kwake


Amefafanua kuwa huduma hizo zitatolewa katika maeneo mbalimbali wakazi wa Mhunze kutakuwa na mabanda maalum katika eneo la Mnadani. na mikutano ya hadhara, Tarafa ya Negezi, huduma zitatolewa katika mabanda yaliyoko Kijiji cha Negezi na mikutano ya hadhara kwenye maeneo mbalimbali na kwa Tarafa ya Mondo, wananchi watafikiwa kupitia mikutano ya hadhara.


Kiongozi wa Timu ya Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Godfrey Ngangaji, amesema lengo kuu la serikali ni kupunguza na hatimaye kuondoa migogoro katika jamii.



“Adhima ya serikali ni kuhakikisha migogoro inapungua au kumalizika kabisa ili wananchi waishi kwa amani na kuendelea na shughuli zao za maendeleo,” ameeleza.


Wananchi wote wa Kishapu wanahimizwa kujitokeza kwa wingi katika kipindi hicho kuanzia Mei 6 hadi 20, 2026, kufika katika maeneo yaliyotengwa ili kuwasilisha migogoro inayowakabiri ili kupatiwa msaada stahiki wa kisheria bila gharama.



Ikumbukwe kuwa hii ni awamu ya pili ya kampeni hii katika Mkoa wa Shinyanga ambapo awamu ya kwanza ilifanyika mwaka 2023, jumla ya migogoro 578 ilishughulikiwa na kati yake migogoro 378 ilitatuliwa, huku zaidi ya wananchi 22,000 wakifikiwa na huduma hiyo.



Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign #MSLAC ) imejikita katika kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi hususan katika masuala ya ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi, mirathi, usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala, na masuala yahusuyo haki za binadamu kwa ujumla.

Katibu Tawala wilayani Fatma Mohamed akifuatilia kwa makini kikao cha wataalamu watakaotekeleza kampeni ya msaada wa kisheria ya
Kiongozi wa timu ya Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Godfrey Ngangaji akizungumza kuhusiana na kampeni ya msaada wa kisheria iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mei 6,2026 Ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya kishapu Mkoani Shinyanga wakati wakielekea kuanza utekelezaji

Msajili Msaidizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Mratibu wa zoezi hilo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Abednego Madole





























Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com