Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JAJI LILA KUONGOZA TUME YA UCHUNGUZI WA JINAI ZA OKTOBA 29, 2025



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumatatu Mei 18, 2026 katika kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Rais ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ameunda Tume itakayoongozwa na Jaji wa Mahakama ya rufani Mhe. Shaban Ally Lila ili kufanya uchunguzi wa kijinai wa matukio ya Oktoba 29, 2025.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozu Balozi Dkt. Moses Kusiluka imesema Rais Samia pia amewateua Mhe. Gad John Mjemmas, Jaji Mstaafu wa Mahakama kuu ya Tanzania, Mhe. Awadh Mohamed Bawazir, Jaji mstaafu wa Mahakama kuu ya Tanzania na Mhe. Aishiel Nelson Sumari, Jaji mstaafu wa mahakama kuu ya Tanzania, kuwa Makamishna wa Tume hiyo.

Kulingana na taarifa ya Balozi Kusiluka, uteuzi huo uliofanywa na Rais Samia umefanyika kwa kuzingatia mamlaka aliyonayo chini ya sheria ya Tume ya uchunguzi, sura ya 32.

Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande alipendekeza kuundwa kwa Tume ya Uchunguzi wa Jinai kwa ajili ya kupeleleza kwa kina matukio mahsusi ya uhalifu yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.Mapendekezo hayo yalitolewa mwezi Aprili 2026 wakati Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani ikikabidhi ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Jaji Chande alifafanua kuwa, ingawa tume yake ilibaini vyanzo na mwelekeo wa jumla wa vurugu za kabla na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, kuna mambo mazito ya kijinai yanayohitaji chombo maalum cha kiuchunguzi ili kuwezesha uwajibikaji wa kisheria.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com