Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Halmashauri ya Jiji la Dodoma imewataka viongozi wa wafanyabiashara wa lililokuwa Soko la Rehema Nchimbi kukaa pamoja na uongozi wa jiji hilo ili kujadili rasimu ya mkataba wa upangaji wa eneo la Umonga, hatua inayolenga kumaliza mvutano unaoendelea kuhusu namna ya kuanza rasmi shughuli za biashara katika eneo hilo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Halmashauri hiyo, Denis Gondwe, amesema kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara hao wakidai kutotendewa haki katika mchakato wa kupatiwa maeneo mbadala baada ya kufungwa kwa soko lao la awali.

Gondwe amesema baada ya kufungwa kwa Soko la Rehema Nchimbi lililokuwa na wafanyabiashara 297 Oktoba mwaka jana, halmashauri ilipendekeza kuwapanga katika masoko mengine, lakini wafanyabiashara walikataa mpango huo.

“Baada ya kukataa kwenda katika masoko yaliyopendekezwa, wafanyabiashara hao waliwasilisha malalamiko yao kwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma wakitaka kupatiwa eneo jingine,” alisema Gondwe.

Alieleza kuwa kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya aliunda kamati maalumu iliyofanya tathmini na kutembelea maeneo mbalimbali, ambapo hatimaye ilipendekeza wafanyabiashara hao wapatiwe eneo lililopo Mtaa wa Kitenge lenye ukubwa wa mita za mraba 8,621.

Gondwe alisema mapendekezo hayo yaliridhiwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kuanza kwa maandalizi ya uendelezaji wa eneo hilo.

Aidha, alisema Waziri Mkuu Mwigulu Lameck Nchemba alipotembelea eneo la Umonga, aliagiza kasi ya utekelezaji iongezwe na kuhakikisha wafanyabiashara wanapatiwa mikataba iliyo wazi kabla ya kuanza shughuli zao.

Kufuatia maelekezo hayo, Gondwe alisema halmashauri iliwaita viongozi wa wafanyabiashara kupitia barua ya Aprili 24, 2026 kwa ajili ya kupitia rasimu ya mkataba wa upangaji, ambapo kikao kilifanyika Aprili 27, 2026.

“Katika kikao hicho, wafanyabiashara walikataa kujadili rasimu ya mkataba,” alisema.

Alisisitiza kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma haitambui ugawaji wowote uliofanyika katika eneo la Umonga, akieleza kuwa yeyote anayedai kupewa eneo hilo nje ya utaratibu rasmi ametapeliwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Jiji la Dodoma, Nsubisi Kapula, alisema serikali iko tayari kuendelea na mazungumzo na viongozi wa wafanyabiashara ili kufikia mwafaka wa pamoja.

Alisema endapo makubaliano hayatapatikana, serikali itaingilia kati na kuhakikisha pande zote zinakutana ili kusaini mikataba rasmi ya uendeshaji wa biashara.

Wakati huo huo, wafanyabiashara hao wameendelea kuiomba serikali kuingilia kati mgogoro huo wakisisitiza kupatiwa eneo la Umonga ili waanze shughuli zao za biashara haraka.

Mvutano huo unaendelea kufuatia kufungwa kwa Soko la Rehema Nchimbi na juhudi za serikali za kuwaweka wafanyabiashara katika maeneo rasmi yenye miundombinu bora ya biashara jijini Dodoma.