Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CRDB BENKI YATOA BILIONI 2.7 KUWASAIDIA ELIMU NA UWEZESHWAJI WANANCHI KIUCHUMI







Na Oscar Assenga,LUSHOTO

Benki ya CRDB imeendelea kudhihirisha dhamira yake ya kuchangia maendeleo ya jamii kwa kutoa zaidi ya shilingi bilioni 2.7 katika mwaka uliopita, fedha ambazo zimeelekezwa kwa kiasi kikubwa katika sekta ya elimu na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vyumba viwili vya madarasa pamoja na ofisi ya walimu katika Shule ya Msingi Kwendoghohi, iliyopo Kata ya Usambara wilayani Lushoto, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Taasisi ya CRDB Bank Foundation, Marian Balampama, alisema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 1 zimetumika kuboresha elimu.

Alieleza kuwa uwekezaji huo umejumuisha ujenzi wa madarasa, ununuzi wa madawati, pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, ikiwemo maabara. Alisisitiza kuwa benki hiyo haijikita tu katika miundombinu, bali pia inahakikisha mwanafunzi anapata mazingira salama na bora ya kujifunzia.



Mbali na elimu, CRDB pia imewekeza katika kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia programu mbalimbali. Balampana alisema benki hiyo inaamini kuwa kumwezesha mtu mmoja ni sawa na kuinua familia na jamii kwa ujumla.

Kupitia kampuni tanzu ya CRDB Bank Foundation na programu ya Embeju, zaidi ya wanufaika 500,000 pamoja na vikundi mbalimbali wamenufaika. Alifafanua kuwa uwezeshaji huo hauishii kwenye utoaji wa fedha pekee, bali pia unahusisha mafunzo ya ujuzi na mbinu za kutambua masoko ili kuongeza tija na faida.



Aidha, alibainisha kuwa benki hiyo imekuwa ikiangalia pia changamoto nyingine za kijamii, ikiwemo upatikanaji wa huduma za afya, kwa lengo la kuboresha ustawi wa wananchi kwa ujumla.

“Sisi tunajisikia fahari kushirikiana na Serikali, hususan katika kusimamia mikopo ya asilimia 10 katika baadhi ya mikoa, ili kuhakikisha fedha zinawafikia walengwa na kuleta matokeo chanya,” alisema Balampana.

Aliongeza kuwa CRDB inaendelea kushirikiana kwa karibu na viongozi wa Wilaya ya Lushoto pamoja na Mkoa wa Tanga katika kutekeleza miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Zephania Sumaye, aliishukuru benki hiyo kwa mchango huo, akisema ujenzi wa madarasa hayo utasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuboresha mazingira ya kujifunzia.



Alieleza kuwa shule hiyo, iliyoanzishwa mwaka 1965, ilikuwa na miundombinu iliyochakaa, hivyo msaada huo unaleta matumaini mapya katika kuinua ubora wa elimu katika eneo hilo.





Kwa ujumla, hatua ya CRDB inaonesha namna taasisi za kifedha zinavyoweza kuwa chachu ya maendeleo kwa kurejesha kwa jamii sehemu ya mapato yao, sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali kufikia dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com