Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CGP KATUNGU - MAFUNZO YA MFUMO WA 'GAMIS' NI UTEKELEZAJI WA MAAGIZO YA RAIS DKT SAMIA




Na. Sgt. Geofrey Jacka - DODOMA

Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, CP.
Nicodemus Tenga, kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Magereza Tanzania, CGP. Jeremiah Yoram Katungu, Mei 19, 2026 amefungua Mafunzo ya Mfumo wa Usimamizi wa Mali za Kudumu za Serikali (GAMIS), akieleza kuwa kufanyika kwa mafunzo hayo ni utekelezaji wa Maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

CP. Tenga amesema, katika kuhitimisha Mafunzo ya Uongozi kwa Maafisa Magereza, Mei 9, 2026 Ukonga Dar Es Salaam, Rais Dkt. Samia, aliekeleza Jeshi la Magereza kutumia TEHAMA katika utendaji wake ili kuongeza ufanisi na uwazi serikalini na kuendana na kasi ya mabadiliko ya Teknolojia.

Aidha, CP. Tenga, amesema ni matarajio ya Jeshi baada ya mafunzo hayo, wataalamu wa ununuzi watakuwa na maarifa mapya ya kutumia mfumo wa GAMIS na kuwaongezea uelewa wa Sheria na Kanuni za usimamizi wa mali za kudumu za Serikali, kuongeza uwajibikaji, kuboresha utunzaji wa kumbukumbu na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za Serikali ikiwemo uhamishaji, uazimishaji na uondoshaji wa mali.

"Ndugu washiriki, majukumu ya ugavi ni mhimili muhimu katika utendaji wa Jeshi, ufanisi wa kazi zenu una mchango mkubwa katika kuhakikisha upatikanaji wa vifaa na huduma muhimu kwa wakati, uwazi na kwa kuzingatia thamani ya fedha, hivyo niwatake muwe makini wakati wote wa mafunzo ili yaweze kuwa na tija" alisema CP. Tenga

Akitoa taarifa ya mafunzo, Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi Jeshi la Magereza, ACP Henry Masawe amesema, Jeshi la Magereza lina jukumu la kutunza na kuhifadhi vifaa na mali zote za kudumu kwa ufanisi na kufuatilia utunzaji sahihi wa kumbukumbu zake hadi pale zitakapo ondoshwa.

Aidha ACP. Masawe, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wagavi kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao kufuatilia na kusimamia mali zote za kudumu za Serikali kwa kutumia mfumo.

Mafunzo hayo ya siku nne ya GAMIS, yanafanyika katika Ukumbi wa Rugimbana jijini Dodoma, yakiweka msisitizo kuwa matumizi ya mifumo ya kisasa ni sehemu muhimu ya kuimarisha uwajibikaji, uwazi na ufanisi katika utendaji wa Jeshi la Magereza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com