Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CCM YAUNGA MKONO MAPENDEKEZO YA MARIDHIANO YA KITAIFA


Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kimetangaza kuunga mkono kwa dhati mapendekezo ya Tume ya Uchunguzi ya Matukio ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 kama hatua ya kuimarisha umoja wa kitaifa.


Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, jijini Dodoma alipokuwa akijibu hoja za viongozi wa Chadema zilizotolewa katika kongamano la wasomi na maazimio ya Kamati Kuu yao.

Kihongosi alisema chama kimepokea ripoti hiyo kwa uzito mkubwa kikiamini kuwa ni chombo muhimu cha kuliponya taifa, huku kikimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha utayari wa kutekeleza mapendekezo hayo. Chama pia kimeunga mkono kuundwa kwa tume ya upelelezi itakayosaidia kubaini ukweli wa matukio ya ghasia yaliyotokea.

Kuhusu suala la Katiba Mpya, CCM imewahakikishia Watanzania kuwa mchakato huo ni ajenda ya chama iliyopo kwenye Ilani na ahadi ya Rais Samia, ikilenga kupatikana kwa Katiba hiyo kabla ya mwaka 2030.

Kihongosi alisisitiza kuwa Katiba si mali ya chama chochote bali ni ya Watanzania wote, hivyo mchakato wake lazima uwe shirikishi. Alihitimisha kwa kusema kuwa hatma ya taifa haiwezi kujengwa kwa misimamo mikali bali kwa maridhiano, kukaa pamoja na kusikilizana ili kudumisha amani na maendeleo ya nchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com