Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CCM YAONYA SIASA ZA MAJITAKA KUVURUGA MAENDELEO YA JAMII



CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeonya tabia ya baadhi ya wananchi kuruhusu itikadi na mipasuko ya kisiasa kuingilia au kuharibu kasi ya maendeleo ya nchi, huku ikionya uwapo wa uchochezi unaopelekea uharibifu wa miundombinu na miradi mikubwa inayotekelezwa na serikali kwa ajili ya manufaa ya jamii.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, alipokuwa akikagua mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Nyasariso iliyopo Kata ya Bunagi, Wilaya ya Tarime mkoani Mara, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa ziara yake ya kikazi ya kukagua uhai wa chama na miradi ya maendeleo mkoani humo.

Akizungumza na wananchi pamoja na wanachama mara baada ya kukagua mradi huo, Kihongosi alisema kumekuwa na wimbi la baadhi ya watu kuendekeza chuki za kisiasa zinazowapelekea kushiriki au kushabikia uharibifu wa mali za umma, jambo ambalo ni kurudisha nyuma uchumi vya taifa.

Alisisitiza kuwa wananchi wa Tarime na Watanzania kwa ujumla wanapaswa kuwa walinzi wa kwanza wa shule, vituo vya afya na miundombinu ya nishati ya umeme, badala ya kuwa wepesi wa kubomoa kwa kufuata mihemko ya wanasiasa.

Kihongosi alibainisha kuwa siasa zinapaswa kufanyika kama uwanja wa kushindanisha hoja na sio jukwaa la kubomoa nchi, akionya kuwa athari za uharibifu huo haziichagui vyama vya siasa bali zinamgusa kila mwananchi.

Alitolea mfano kuwa kitendo cha kuchoma moto shule kinawaumiza watoto wa masikini wanaolazimika kurudi nyumbani, huku uharibifu wa vituo vya afya au kukatwa kwa nguzo za umeme ukisimamisha mnyororo mzima wa uzalishaji kiuchumi na kuhatarisha maisha ya wagonjwa.


Katika ziara hiyo, viongozi wa chama walipokea taarifa ya mradi kutoka kwa Mkuu wa Shule hiyo ya Sekondari ya Nyasariso, Paschal Sobu, ambaye alieleza kuwa shule hiyo ya mchanganyiko inayochukua wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita imejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.6.


Sobu alifafanua kuwa katika kiasi hicho cha fedha, serikali kuu ilichangia shilingi bilioni moja wakati kiasi kilichobaki cha zaidi ya shilingi milioni 600 kikitokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.


Mkuu huyo wa shule aliongeza kuwa miundombinu iliyopo inajumuisha madarasa 13, ofisi tano za walimu, jengo la utawala, maabara za kisasa za masomo ya kemia na baiolojia, bwalo la chakula pamoja na jiko la kisasa linalotumia nishati safi ya kupikia.


Alibainisha kuwa kwa sasa shule hiyo ina jumla ya walimu 13, wakiwemo wanaume 10 na wanawake watatu, kukiwa na mwalimu mmoja wa kujitolea anayelipwa kupitia ushirikiano wa karibu kati ya wazazi na halmashauri hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com