Mchambuzi wa masuala ya siasa na Diplomasia Dkt. Dennis Muchunguzi amesisitiza umuhimu wa utulivu kwa Watanzania katika kusubiri ripoti ya Tume huru ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani ya wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2026, badala ya kuanza kuzusha uongo dhidi ya ripoti hiyo na Tume hiyo ambayo bado haijakamilisha kazi yake.
Muchunguzi amebainisha hayo leo Jumatatu Aprili 13, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar Es Salaam, akisema mpaka sasa hakuna anayefahamu maudhui ya ripoti hiyo, suala ambalo linalazimisha kila mmoja kuwa na subira kusubiri utekelezaji wa hadidu za rejea zilizotolewa kwa Tume hiyo kama muongozo wa utendaji wake wa kazi.
"Sisi ni Taifa ambalo lina amani, umoja, muungano na mshikamano. Baada ya ripoti ile kama Taifa tunatakiwa kuendelea kushikamana na kuvumiliana kama ilivyo falsafa ya maridhiano ya Rais Samia ya R4 ya kuvumiliana na kustahimiliana na tujue sisi ni binadamu bado, tunaweza kufanya makosa na tunatakiwa kuwa watu wa kusameheana." Amesema Muchunguzi.
Katika maelezo yake, Mchambuzi huyo amesema ikiwa Taifa litaenda kwa tabia ya kusameheana pamoja na kujisahihisha, Taifa litaendelea kuwa na umoja na lenye ustawi kwa kila mmoja, akisema yaliyotokea Oktoba 29, 2025 ni muhimu kuhakikisha hayarejei tena licha ya kuwa hayawezi kufutwa katika historia ya Tanzania, akimtaka kila mmoja kuiishi falsafa ya Rais Samia ya 4R kama msingi wa kuendeleza umoja na mshikamano wa Watanzania.

Social Plugin