Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuhakikisha matumizi bora na salama ya nishati nchini kwa kuandaa viwango vya ufanisi wa nishati vinavyolenga kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kulinda mazingira.
Akizungumza leo Aprili 13, 2026 jijini Dar es Salaam, Afisa Viwango wa TBS, Mhandisi Spiradson Kagaba, amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia uliozinduliwa mwaka 2024 pamoja na Mkakati wa kitaifa wa matumizi sanifu ya nishati uliozinduliwa mwaka huo huo, 2024 .
Amesema mkakati wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia una lengo la kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya kaya nchini zinatumia nishati safi ya kupikia.
“Pamoja na mkakati huo, Serikali inalenga kuongeza ufanisi wa matumizi ya nishati kupitia mkakati wa kitaifa wa matumizi sanifu ya nishati kwa lengo la kupunguza upotevu wa nishati, kulinda vyanzo vya nishati na kufikia malengo ya maendeleo endelevu (SDGs),” amesema Kagaba.
Amefafanua kuwa TBS, kama msimamizi wa viwango nchini, imeandaa viwango vya chini vya ufanisi wa nishati (Minimum Energy Performance Standards - MEPS) vinavyotumika kudhibiti ubora wa vifaa vinavyotumia nishati.
Kwa mujibu wa Kagaba, viwango hivyo vinahusisha vifaa mbalimbali vya majumbani ikiwemo majiko banifu, majiko ya umeme, majokofu (refrigerators), viyoyozi (air conditioners), mota za umeme, taa, runinga pamoja na feni.
“Lengo la viwango hivi ni kuhakikisha vifaa vinavyotumika na wananchi vinatumia nishati kwa ufanisi mkubwa, hivyo kupunguza matumizi ya umeme na gharama kwa mtumiaji,” ameeleza.
Aidha, amesema TBS imejenga maabara za kisasa, maalum kwa ajili ya kupima na kuthibitisha ubora wa vifaa hivyo kabla ya kuruhusiwa kuingia sokoni.
Amesema kuwa bila kuzingatia viwango vya ufanisi, matumizi ya umeme nchini yanaweza kuongezeka kwa asilimia 87 ifikapo mwaka 2030, hali ambayo italazimu uwekezaji mkubwa katika uzalishaji wa umeme na kuongeza gharama kwa Serikali.
“Badala ya kuongeza uzalishaji wa umeme ambao ni gharama kubwa na wakati mwingine si rafiki kwa mazingira, ni bora kudhibiti matumizi kupitia ufanisi wa vifaa,” amesema.
Kagaba ameongeza kuwa vifaa vyote vinavyozalishwa nchini au kuingizwa kutoka nje vitatakiwa kukidhi viwango vilivyowekwa, vinginevyo havitaruhusiwa kuuzwa sokoni.
Katika hatua nyingine, TBS imeanzisha mfumo wa lebo za ufanisi wa nishati zitakazowekwa kwenye vifaa ili kumsaidia mnunuaji kufanya maamuzi sahihi.
Ameeleza kuwa lebo hizo zitaonesha kiwango cha matumizi ya nishati kwa mfumo wa nyota, ambapo kifaa chenye nyota nyingi kina ufanisi mkubwa zaidi na hutumia umeme kidogo.
“Kwa mfano, kifaa chenye nyota tano kinatumia umeme kidogo zaidi kuliko cha nyota nne, tatu au mbili, hivyo kumwezesha mtumiaji kuokoa gharama za umeme kwa muda mrefu,” amesisitiza.
Hatua hiyo inatarajiwa kusaidia si tu kupunguza matumizi ya nishati bali pia kuhamasisha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira na kuchochea maendeleo endelevu nchini.

Social Plugin