Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SOVELLA AWAHAKIKISHIA WANANCHI WA MSHANGANO MAENDELEO ASIKILIZA KERO ZAO ANA KWA ANA

Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Mshangano Benson Sovella akiwa anazungumza leo tarehe 26 aprili 2026 mtaa wa Chandarua wakati wa ziara yake ya kuwashukuru wananchi na wajumbe waliomchagua katika kipindi cha uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 29 Oktoba 202Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Mshangano Benson Sovella akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa kata ya Mshangano wakati wakisikiliza hoja za wananchi wakati wa ziara yake 


Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma 


Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Mshangano, Benson Sovella, ameanza ziara maalum katika mitaa ya Mshangano, Namanyigu, Mitendewawa, Chandarua na Muhombezi kwa lengo la kuwashukuru wananchi pamoja na wajumbe waliomchagua, huku akisisitiza dhamira yake ya kuwatumikia bila ubaguzi. 


Akiwa katika mtaa wa Chandarua, Sovella amewashukuru wananchi kwa imani kubwa waliyoonyesha kwake, akieleza kuwa ushindi wake umetokana na mshikamano wao, hata katika nyakati ngumu walizokumbana nazo. 


Ameahidi kuwa diwani wa watu wote na kusisitiza kuwa yupo tayari kusimama bega kwa bega na wananchi katika kutatua changamoto zao.


Katika mazungumzo yake, Sovella amegusia kwa kina changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, hususani  miundombinu ya barabara, huduma ya maji na umeme. 


Kuhusu maji, ameeleza kuwa kuna mkakati wa kuboresha upatikanaji wake kwa kushirikiana na mamlaka husika, ikiwa ni pamoja na kuondokana na matumizi ya nishati ya sola na badala yake kutumia umeme ili kuongeza nguvu ya usambazaji. 


Amebainisha kuwa mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa katika miji 28, ukiwemo Manispaa ya Songea, ukikamilika utahakikisha upatikanaji wa maji kwa zaidi ya asilimia 85 ya wakazi wa kata hiyo, huku tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni mbili kwa siku likitarajiwa kuondoa kabisa changamoto hiyo.


Aidha, Sovella amezungumzia maendeleo katika sekta ya afya na usafiri, akitaja umuhimu wa zahanati ya Chandarua inayohudumia wakazi wa maeneo jirani. 


Amekiri kuwepo kwa changamoto ya barabara mbovu na vivuko, lakini amewahakikishia wananchi kuwa tayari bajeti ya kuboresha miundombinu hiyo imetengwa. 


Kuhusu umeme, ameeleza kuwa juhudi zinaendelea kuhakikisha maeneo yote yanapatiwa huduma hiyo, huku changamoto za gharama na upatikanaji wa nguzo zikifanyiwa kazi.


Kwa upande wao, baadhi ya wananchi akiwemo Esta Nyoni na John Ngonyani wamempongeza diwani huyo kwa kuwajali na kusikiliza kero zao, wakiahidi kushirikiana naye katika kuleta maendeleo. 


Hata hivyo, wamewasilisha ombi la kufunguliwa kwa barabara muhimu zinazounganisha Chandarua na Shule ya Tanga pamoja na kutoka Muhombezi hadi Machinjioni, wakieleza kuwa hali ya sasa inalifanya eneo hilo kuwa kama kisiwa. 


Wananchi pia wamelalamikia ubovu wa barabara na changamoto za malipo ya umeme, wakitarajia kuwa ziara ya diwani huyo imeleta suluhisho baada ya majibu waliyoyapokea kwa kile walichojibiwa na Mheshimiwa diwani na kuwa na nguvu na matumaini ya changamoto hizo kutatuliwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com