Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wamehimizwa kuendelea kuulinda na kuuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa misingi ya undugu, uzalendo, amani na mshikamano ili kudumisha tunu hiyo adhimu ya Taifa.
Wito huo umetolewa leo Aprili 26, 2026 na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Mboni Mhita, wakati wa sherehe zaa maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano yaliyofanyika katika Wilaya ya Kishapu. Akiwa mgeni rasmi wa maadhimisho hayo amesisitiza kuwa Muungano huo umeweka historia ya kipekee si tu barani Afrika bali pia duniani.
“Muungano wetu ni hazina ya Taifa letu ni daraja la umoja, nguzo ya amani, na msingi wa maendeleo. Ni wajibu wetu sote kuuenzi kwa vitendo, kuurithisha kwa vizazi vijavyo, na kuulinda kwa nguvu zote ili uendelee kuwa alama ya mshikamano wa Watanzania.” ameongeza Mhita
Katika kuadhimisha siku hiyo, ameshiriki zoezi la usafi wa mazingira pamoja na kutembelea wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ambapo amesisitiza umuhimu wa usafi katika kuzuia magonjwa malaria na magonjwa mengine ya mlipuko ya kuhara na kutapika.
Ameeleza kuwa wananchi wanaendelea kunufaika na maboresho makubwa katika sekta ya afya yanayotokana na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia uwekezaji mkubwa katika miundombinu, vifaa tiba na huduma za kisasa.
“Tumeshuhudia wenyewe hali ya utoaji huduma hospitalini hapa ni bora, salama na kwa wakati. Haya ni matokeo ya uwekezaji mkubwa wa Serikali katika sekta ya afya,” ameongeza Mhita.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa ameshiriki zoezi la upandaji miti na kuweka jiwe la msingi katika mradi mpya wa vyumba vya madarasa ya awali na msingi katika Shule ya Sekondari Isoso, ambapo amewahimiza wanafunzi kusoma kwa bidii ili kufikia ndoto zao na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Katika hatua nyingine, ameipongeza Wilaya ya Kishapu kwa juhudi zake katika upandaji miti na kuhifadhi mazingira, akizitaka halmashauri nyingine mkoani Shinyanga kuiga mfano huo ili kulinda mazingira kwa maendeleo endelevu.
Akihitimisha maadhimisho hayo yaliyofanyika katika Viwanja vya Michezo shule ya msingi Buduhe, Mhe. Mhita amewakumbusha wananchi umuhimu wa kudumisha amani na kuuenzi Muungano kwa vitendo, huku akieleza kuwa mafanikio ya Taifa yanategemea umoja na mshikamano wa watu wake.
Baadhi ya wagonjwa wamethibitisha kupokea huduma nzuri hospitalini hapo huku wakimuomba Mkuu huyo kufikisha salamu kwa Mhe. Rais za kuendelea kuwekeza zaidi kwenye sekta ya afya kwa kuedelea kuajiri watumishi na upatikanaji wa dawa kuongezeka.
Maadhimisho hayo yameacha ujumbe mzito wa uzalendo, yakikumbusha kuwa Muungano si historia tu, bali ni urithi hai unaopaswa kulindwa na kila Mtanzania.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita akizungungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya michezo shule ya Msingi Buduhe Kata ta ya Kishapu wilayani Kishapu mkoani humo wakati wa sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kimkoa Aprili 26,2026
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi akizungumza kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano huku Wilaya ya Kishapu ikiwa ni mwenyeji wa maadhimisho hayo kimkoa Aprili 26, 2026
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Josephat Limbe
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Emmanuel Johnson
Muonekano wa picha ya juu wa Shule ya awali, msingi na sekondari Isoso iliyoko Kata ya Kishapu wilayani Kishapu mkoani Shinyanga
Social Plugin