Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

'MAPENDEKEZO YA TUME NI DAWA CHUNGU, LAZIMA INYWEWE KULIPONYA TAIFA'

 

Katika kile kinachoonekana kama mwanzo wa ukurasa mpya wa siasa na amani nchini Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan amepokea ripoti ya Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Oktoba 29, 2025, kwa kauli nzito ya ujasiri na uwajibikaji. 

Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam jana baada ya kupokea matokeo ya kazi hiyo ya siku 153, Rais Samia alifananisha mapendekezo ya tume hiyo na dawa ambayo taifa halina budi kuinywa ili kupata uponyaji wa kudumu. 

"Mapendekezo mliyotoa ni dawa ya kuliponya taifa letu, na kwa ladha yoyote iliyo dawa hiyo, lazima inywewe ili tupone," alisema Rais kwa msisitizo, akionyesha utayari wa serikali yake kutekeleza kila hatua iliyopendekezwa bila kusita.

Rais Samia, kwa hisia kali, alikiri kuwa machafuko hayo yaliyotikisa misingi ya nchi ni doa ambalo hakutegemea lingetokea wakati wa uongozi wake, akieleza kuwa jambo hilo limemtwisha "mzigo mzito" ambao ameapa kuubeba kwa ujasiri na tahadhari kubwa. 

Alibainisha kuwa matukio hayo hayakuwa ya bahati mbaya, bali yalipangwa na kuratibiwa na watu wenye nia ovu ya kudhoofisha serikali, kuvuruga uchaguzi, na kuhujumu miundombinu muhimu ya uchumi. 

Hata hivyo, alisisitiza kuwa sasa ni wakati wa Watanzania kutumia doa hilo kama hatua muhimu ya kurejesha umoja na mshikamano, akiahidi kufanya marekebisho makubwa kwenye maeneo yaliyobainika kuwa na dosari na kuwawajibisha wote waliohusika na kadhia hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com