Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JAJI CHANDE APASUA JIPU;HAKUNA MAKABURI YA HALAIKI WALA UTESAJI DAR

Tume ya uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani imetoa majibu ya kisayansi na kiuchunguzi kufuatia madai yaliyosambaa kimataifa na kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kuwepo kwa makaburi ya halaiki katika Manispaa ya Kinondoni. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hakuna ushahidi wowote wa kuwepo kwa makaburi ya namna hiyo katika maeneo ya Kondo na Kunduchi kama ilivyokuwa ikivuma.

Ili kufikia tamati ya utata huo, Tume ilifanya uchunguzi wa kina ulioshirikisha wataalamu wa uchambuzi wa mbali na mifumo ya taarifa za kijiografia (Remote Sensing and GIS). Wataalamu hao walitumia picha za satelaiti kulinganisha muonekano wa maeneo hayo kabla na baada ya ghasia, ambapo hakuna mabadiliko yoyote ya ardhi yanayoashiria kuchimbwa kwa mashimo makubwa ya halaiki yaliyobainika.

Pamoja na matumizi ya teknolojia, Tume ilitembelea maeneo yote yaliyotajwa na kufanya mahojiano ya ana kwa ana na wasimamizi wa makaburi ya manispaa hiyo. Ushahidi wa Afisa Msimamizi wa makaburi ya Kinondoni na msimamizi wa makaburi ya Kondo ulithibitisha kuwa hakuna shughuli yoyote isiyo ya kawaida ya maziko iliyofanyika katika kipindi hicho cha ghasia za uchaguzi.

Tume imesema madai ya watu kuteswa wakati wa ghasia hizo hayana ushahidi. Imeelezwa kuwa hakuna ushahidi wa mtu yeyote aliyefikishwa mbele ya tume au kubainika kupitia vyanzo vingine kuwa alifanyiwa vitendo vya utesaji. 

Hatua hii ya Tume kuweka wazi matokeo ya uchunguzi wa kisayansi inalenga kufuta upotoshaji uliokuwa umeanza kuipaka matope taswira ya nchi katika anga la kimataifa, huku ikisisitiza kuwa uamuzi wa Rais Samia kuunda tume hiyo umesaidia kuleta ukweli na uwazi mbele ya jamii ya kimataifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com