Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JAJI CHANDE ATAJA VYANZO VYA MSINGI VYA USHIRIKI GHASIA

Wakati ghasia za Oktoba 2025 zikionekana kuwa na sura ya kisiasa, Tume ya Jaji Othman Chande imebaini vyanzo vitano vya ndani vilivyotoa mpenyo kwa matukio hayo, huku ugumu wa maisha na kero za kijamii zikichukua nafasi kubwa. Ripoti hiyo imeainisha kuwa ghasia hizo zilichangiwa na mchanganyiko wa malalamiko ya kisiasa, kiuchumi, na utendaji mbovu wa baadhi ya watumishi wa umma.

Katika upande wa kisiasa, Jaji Chande alibainisha kuwa madai ya Katiba Mpya, hitaji la demokrasia pana katika mfumo wa vyama vingi, na malalamiko ya uboreshaji wa Tume Huru ya Uchaguzi yalikuwa miongoni mwa vyanzo vikuu. Mashahidi waliofika mbele ya tume hiyo walieleza kuwa kutopatiwa ufumbuzi kwa mambo hayo kulijenga kutoridhika kwa muda mrefu miongoni mwa wadau.


Hata hivyo, ripoti imeweka uzito mkubwa katika masuala ya kijamii na kiuchumi. Jaji Chande alitaja ugumu wa maisha, ukosefu wa ajira, na kukosekana kwa usawa katika fursa za kiuchumi kama baruti iliyosubiri kiberiti. Aidha, mazingira magumu ya biashara, utitiri wa tozo na kodi, pamoja na mfumo usio rafiki wa ukusanyaji kodi, vilitajwa kuwaumiza wananchi wengi na kuwafanya wawe tayari kushiriki katika machafuko.

Ripoti pia imemulika mmomonyoko wa maadili na kushuka kwa uzalendo, huku ikibainisha kuwa kero za rushwa, madai ya utekeji, na kupotea kwa watu vilipokosa majibu stahiki kutoka serikalini, viliongeza chuki dhidi ya mamlaka. Jaji Chande aliongeza kuwa utendaji mbovu wa watumishi wa ngazi za chini, hasa katika serikali za mitaa ambao hawakusikiliza kero za wananchi, ulichochea wananchi kuona vurugu ndiyo njia pekee ya kusikilizwa.

Ha hivyo tume hiyo ilionya kuhusu maslahi ya mataifa ya nje. Jaji Chande alisema mataifa mengi yanatanguliza maslahi yao katika nchi zenye rasilimali nyingi kama Tanzania, jambo ambalo linaweza kuchangia kuyumba kwa amani ya ndani ikiwa vyanzo vya ndani havitatatuliwa kwa wakati na kupitia utekelezaji wa mapendekezo ya tume mbalimbali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com