Dar es Salaam, Aprili 13 2026:
Katika kipindi cha mwezi Machi 2026, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 1,983.31 za dawa mbalimbali za kulevya, kilogramu 3,012.5 na lita 17,960 za kemikali bashirifu, vidonge 286 na chupa 1,001 za dawa tiba zenye asili ya kulevya. Sambamba na ukamataji huo, ekari 55.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa huku watuhumiwa 77 wakikamatwa kuhusiana na makosa hayo. Katika matukio hayo, magari tisa, pikipiki 12 na bajaji moja vilikamatwa.
Uchambuzi wa takwimu umebaini ongezeko la ukamataji wa dawa za kulevya aina ya mirungi, ambapo kilogramu 1,267.12 zilikamatwa, sawa na 64 ya dawa zote zilizokamatwa mwezi huo. Hali hii imetokana na mkakati wa Mamlaka kujikita katika operesheni za dawa za kulevya za mashambani baada ya kudhibiti kwa kiasi kikubwa mitandao ya dawa za kulevya za viwandani.
Baadhi ya matukio ya ukamataji yaliyofanyika katika maeneo mbalimbali nchini ni kama ifuatavyo:
Jijini Dar es Salaam, katika eneo la Tegeta Kibo, kilogramu 101.2 za mirungi zilikamatwa zikiwa zimefichwa katika basi la abiria aina ya Yutong la kampuni ya Abood lenye namba ya usajili T 181 EMJ lililokuwa likifanya safari kati ya Mombasa, Kenya na Dar es Salaam, Tanzania.
Dawa hizo zilifichwa katika maeneo mbalimbali ya basi hilo ikiwemo ndani ya mfumo wa hewa (AC) kwa lengo la kukwepa kugundulika. Watuhumiwa waliokamatwa katika tukio hilo ni dereva wa basi hilo Ramadhan Mohamed (52), Salma Sanga (26) kondakta, Twahilu Athuman (38), Mohamedy Mikidadi (37) na Ibrahim Mohamed (39). Mkoani Pwani kilogramu 419.09 za mirungi zilikamatwa zikiwa zinasafirishwa kuelekea Dar es Salaam.
Mkoani Mwanza, zilikamatwa kilogramu 52 za mirungi katika kizuizi cha barabarani cha Magu pamoja na Bandari ya Mwanza South, ikisafirishwa kwa kutumia gari aina ya Fuso yenye namba ya usajili T 296 APA. Dawa hizo zilikuwa zimefichwa katikati ya mizigo mingine, ikiwemo mabelo ya nguo za mitumba. Dereva wa gari hilo, Hassan Hassan (37), mkazi wa Mahina Nyamagana alikamatwa.
Aidha, wilayani Misungwi mkoani humo, kilogramu 184.9 za mirungi zilikamatwa zikiwahusisha watuhumiwa Chrispin Shoo (62) na mkewe Esther Pastory (55). Dawa hizo zilibainika ndani ya nyumba na katika vyombo vya usafiri ambavyo ni Gari aina ya Toyota Crown yenye namba ya usajili T 742 EGL, Toyota Wish yenye
namba ya usajili T 854 DXB, pamoja na bajaji yenye namba za usajili MC 261 EZV.
Mkoani Tanga, zilikamatwa Kilogramu 32.95 za Mirungi ikiwa imefichwa ndani ya mfuko kwa kuchanganywa na maembe. Katika tukio hilo, Seif Omar (38), maarufu kwa jina la Haniwao, mkazi wa Mtaa wa Taifa Barabara ya 13, ambaye pia ni mjumbe wa Serikali ya Mtaa alikamatwa. Katika operesheni nyingine zilizofanyika mkoani humo, jumla ya Kilogramu 164.01 za Mirungi zilikamatwa katika matukio tofauti.
Vilevile, mkoani Arusha, katika wilaya ya Longido, Kilogramu 106.25 za Mirungi zilikamatwa zikiwa zinasafirishwa kwa gari aina ya Toyota Wish yenye namba ya usajili T 889 DPG. Katika tukio hilo, watuhumiwa Solomon Koholo (38), Diwani wa Kata ya Kimokouwa pamoja na Lekaneti Kukuu (38) walikamatwa.
Aidha, Kilogramu 138.42 za dawa za mirungi zilikamatwa katika matukio mengine yaliyofanyika mkoani humo.
Kadhalika mkoani Kilimanjaro, katika eneo la Himo na Same, Kilogramu 68.3 za mirungi zilizowahusisha watuhumiwa Amin Mazua (58) maarufu kwa jina la Mbaruku na Wilbard Mchau (50).
Sambamba na udhibiti wa mirungi, aina nyingine ya dawa za kulevya zilikamatwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Jijini Dar es Salaam, kwenye hosteli ya wanafunzi iliyopo mtaa wa Nzasa, Kijitonyama zilikamatwa Paketi 141 za bangi aina ya skanka. Katika tukio hilo, alikamatwa mtuhumiwa Semvua Sangi (31), msimamizi wa hosteli hiyo ambaye dawa hizo zilipatikana ndani ya chumba chake katika hosteli hiyo.
Tukio hili linaashiria uwepo wa mienendo ya biashara ya dawa za kulevya katika maeneo yanayozunguka taasisi za elimu. Mamlaka inatoa wito kwa jamii, hususani wamiliki na wasimamizi wa makazi ya wanafunzi, kushirikiana na vyombo vya dola kuhakikisha mazingira ya wanafunzi yanabaki salama bila dawa za kulevya.
Aidha, mkoani Songwe katika eneo la Tunduma, zilikamatwa Kilogramu 8.2 za bangi aina skanka.
Dawa hizo zilibainika zikiwa zinasafirishwa na mtuhumiwa Lwitiko Kapambila (39) kuelekea Mbeya mjini, akiwa ndani ya lori aina ya FAW alilokuwa ameomba lifti kutokea Tunduma.
Katika operesheni nyingine zilizofanyika nchini, jumla ya kilogram 707.995 za bangi zilikamatwa.
Katika kuimarisha udhibiti wa kemikali bashirifu na kuzuia uchepushwaji wa dawa tiba zenye asili ya kulevya, Mamlaka kwa kushirikiana na Mamlaka nyingine za udhibiti ilifanya ukaguzi katika kampuni zinazojihusisha na
kemikali bashirifu, maduka ya dawa tiba, kampuni za usafirishaji vifurushi na bandari kavu.
Kutokana na ukaguzi huo, jumla ya kilogramu 3,012.5 na lita 17,960 za kemikali bashirifu zilizuiliwa kutokana na kukiuka taratibu mbalimbali za kisheria. Miongoni mwa Kemikali hizo ni Potassium permanganate, Hydrochloric acid, Acetone, Sulphuric acid, na Acetic acid glacial.
Kemikali hizi endapo zingechepushwa zingeweza kutumika katika mchakato wa kuzalisha dawa za kulevya.
Aidha, kupitia ukaguzi huo, vidonge 286 na chupa 1,001 za dawa tiba zenye asili ya kulevya vilikamatwa. Dawa hizo ni alprazolam, midazolam, clonazepam, Fentanyl, zolpidem, Tramadol, Codeine na dihydrocodeine.
Kitaalam, dawa hizi zinajumuisha makundi ya Benzodiazepini, dawa za kutuliza na kusababisha usingizi, pamoja na dawa zenye asili ya afyuni ambazo hutumika kutibu maumivu.
Endapo matumizi ya dawa hizi hayatadhibitiwa ipasavyo zinaweza kusababisha uraibu na utegemezi kwa mtumiaji sawa na dawa za kulevya.
Kwa ujumla, operesheni za mwezi Machi, 2026 zimeakisi dhamira thabiti ya Serikali katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya nchini.
Pamoja na dhamira hiyo, mwenendo wa ukamataji unaonesha uwepo wa mitandao mipya ya usafirishaji wa dawa za kulevya hususan mirungi, pamoja na kubadilishwa kwa mbinu za usafirishaji ili kukwepa kubainika, hata hivyo, Mamlaka inaendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, taasisi nyingine za udhibiti, wadau na wananchi kwa ujumla ili kudhibiti mianya yote inayoweza kutumiwa na wahalifu wa dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua kali za kisheria kwa mtu yeyote atakayebainika
kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya bila kujali hadhi au nafasi yake katika jamii.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
MAMLAKA YA KUDHIBITI NA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA.


.jpeg)










Social Plugin