Na Kadama Malunde – Malunde 1 Blog
Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, amekagua na kuthibitisha kukamilika kwa asilimia 99 kwa Mradi wa Ujenzi wa Daraja la Mwabomba, mradi ambao umeendelea kuibua furaha kwa wananchi kutokana na kuondoa adha ya muda mrefu ya kuvuka katika eneo hilo, hususan wakati wa masika.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo iliyofanyika Jumatatu Aprili 13, 2026 katika Kata ya Idahina, Halmashauri ya Ushetu, Mhe. Cherehani amesema daraja hilo lenye gharama ya shilingi bilioni 2.2 sasa limeanza kutumika rasmi na limekuwa mkombozi kwa wananchi wa Mwabomba, Masumbwe na maeneo jirani.
“Daraja la Mwabomba limekamilika kwa asilimia 99, yamebaki marekebisho madogo madogo kama kuweka alama na kazi za mwisho za mkandarasi. Lakini sasa wananchi wanapita bila shida, bila hofu yoyote. Hii ni hatua kubwa sana kwa maendeleo ya Ushetu,” amesema Cherehani.
Ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha miundombinu ya usafiri, hasa maeneo yaliyokuwa yakikumbwa na changamoto kubwa wakati wa mvua.
“Mradi huu ni utekelezaji wa maono ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata miundombinu imara. Hapa Mwabomba tulikuwa na kero kubwa sana kipindi cha masika, sasa historia imebadilika,” ameongeza.
Akifafanua zaidi, Mbunge huyo amesema wananchi wa maeneo ya Masumbwe na Mwabomba walikuwa wakikumbwa na changamoto kubwa ya kuvuka kutokana na maji kufunika daraja la zamani, hali iliyokuwa ikiathiri shughuli za kiuchumi na kijamii.
“Daraja hili lilikuwa kero na maumivu makubwa kwa wananchi. Kipindi cha masika watu walikuwa wanateseka, wengine wakishindwa kuvuka kabisa. Leo hii tunashuhudia mabadiliko makubwa – wananchi wanavuka kwa amani na uhakika,” amesema.
Sambamba na mradi wa daraja, Mhe. Cherehani ametembelea eneo la ujenzi wa Kituo cha Afya Idahina kilichopo kijiji cha Mwabomba, ambapo ameshiriki zoezi la ufyatuaji matofali na kukabidhi shilingi milioni 650 kwa ajili ya kuharakisha ujenzi huo.
“Tuliwaahidi wananchi kituo cha afya na leo tumetekeleza. Nimekuja na shilingi milioni 650 na tayari milioni 250 zipo kwenye akaunti. Nataka ujenzi uanze mara moja ili wananchi waanze kupata huduma karibu yao,” amesema.
Aidha, amesisitiza kuwa serikali tayari imeshatenga fedha kwa ajili ya vifaa tiba, huku akiahidi kufuatilia upatikanaji wa gari la wagonjwa ili kuboresha huduma za afya mara baada ya mradi kukamilika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, amepongeza utekelezaji wa miradi hiyo, akieleza kuwa Daraja la Mwabomba ni ushahidi wa wazi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM na dhamira ya serikali kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.
“Daraja la Mwabomba sasa linapitika bila hofu. Hili ni jambo la kihistoria kwa wananchi wa hapa. Wananchi wanavuka bila shida, bila uoga wowote,” amesema Mlolwa.
Ameongeza kuwa mradi huo umeondoa kabisa changamoto ya muda mrefu ya usafiri, hususan kipindi cha mvua, na sasa umefungua fursa za kiuchumi kati ya Mwabomba, Masumbwe, Urambo, Kaliua hadi Geita.
Mradi wa Daraja la Mwabomba, uliotekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), umeendelea kusifiwa kuwa miongoni mwa miradi iliyobadili maisha ya wananchi wa vijijini kwa kuimarisha usafiri, biashara na usalama wa wananchi katika maeneo ya mto huo.

Wakazi wa Mwabomba, Juma Mwendesha Nigula na Doha Masalu, wamesema kuwa awali wananchi walikuwa wakikumbana na changamoto kubwa ya kuvuka daraja hilo hasa wakati wa masika, ambapo maji yalikuwa yakifunika daraja la zamani na kusababisha adha kubwa kwa wasafiri na wakazi wa eneo hilo.
Wamesema hali hiyo ilikuwa ikiathiri shughuli za kijamii na kiuchumi, lakini sasa mabadiliko makubwa yamepatikana baada ya ujenzi wa daraja jipya kukamilika, hatua ambayo imeleta faraja na usalama kwa wananchi.
“Kipindi cha masika daraja la mwanzo lilikuwa linafunikwa na maji mengi, hali iliyokuwa ikitutesa sana. Leo tunatoa shukrani kwa mbunge na Rais Samia kwa kuendelea kutatua changamoto za wananchi. Sasa tunavuka bila hofu,” amesema Nigula.














@malundeblog Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mhe. Emmanuel Cherehani amefanya mkutano mkubwa wa kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kuwa Mbunge. Akiwa ameambatana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mabala Mlolwa, Mbunge Cherehani amesherehekea Siku ya Kuzaliwa na Wananchi wa Kijiji cha Mwabomba kata ya Idahina. Hali kadhalika amekagua daraja la Mwabomba ambalo limekamilika kwa asilimia 99 pamoja na kukabidhi fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Mwabomba! Tazama hivi Vibe!!
♬ original sound - Malunde
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com
Social Plugin