Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CCM YATAKA ENEO YA KUKUSANYIA TAKA SOKO LA MGANDINI LIBORESHWE





Na Oscar Assenga, TANGA

Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga kimetoa maelekezo kwa Halmashauri ya Jiji la Tanga kuhakikisha maeneo ya kukusanyia taka katika soko la Mgandini yanaboreshwa kwa kujazwa kifusi ikiwemo kurekebisha barabara za ndani ili kuimarisha usafi.

Agizo hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Rajab Abdurhaman wakati wa ziara yake ambapo alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha maji ya mvua yanaelekezwa ipasavyo kwenye mifereji ili kuepusha mafuriko na uharibifu wa miundombinu.



Ziara hiyo ilikuwa ni kufuatilia utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa awali kuhusu kuboresha usafi wa soko hilo ambapo viongozi wa Jiji hilo walianza kuyafanyia kazi ikiwemo kuondosha uchafuzi uliokuwepo awali.

Awali, wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya usafi, Mwenyekiti huyo hakuridhishwa na mazingira ya soko hilo na kutoa muda wa mwezi mmoja kwa uongozi wa Jiji kuhakikisha hali ya usafi inaboreshwa.

Akizungumza baada ya kufanya ziara ya ufuatiliaji, Rajab aliwapongeza Mstahiki Meya pamoja na viongozi wa Jiji kwa kuchukua hatua na kuanza kutekeleza maelekezo hayo ya CCM.

“Hatuhitaji viongozi wa kulalamika, tunahitaji viongozi wanaochukua hatua kutatua changamoto za wananchi. Mlichokifanya ni kutimiza wajibu wenu,” alisema.

Alisema kuwa hali ya uchafu iliyokuwepo awali haikuwafurahisha viongozi wala wafanyabiashara, hivyo hatua zilizochukuliwa zinaonesha uwajibikaji wa uongozi.

Hata hivyo Mwenyekiti Rajab alisisitiza kuwa atarejea kukagua maendeleo hayo baada ya wiki mbili na kuonya kuwa hataki kusikia visingizio badala ya utekelezaji.

“Ndani ya mwezi mmoja kuanzia Aprili 9 hadi Mei 9, tunatarajia kuona kazi imeanza. Hatutaki hadithi, tunataka vitendo,” alisisitiza.

Aidha, alieleza kuwa Jiji la Tanga ni taswira ya mkoa huo, hivyo linapaswa kuwa safi na lenye mpangilio mzuri.

Alikumbusha kuwa zamani Tanga ilikuwa mji unaojulikana kwa usafi na ustaarabu, hivyo ipo haja ya kurejesha hali hiyo.

Kuhusu huduma za vyoo katika soko hilo, Mwenyekiti alieleza kutoridhishwa na hali iliyopo, akibainisha kuwa choo kilichopo hakitoshelezi mahitaji kutokana na idadi kubwa ya watumiaji.

Alisema kuwa hali hiyo inasababisha baadhi ya watu kulazimika kujisaidia katika maeneo yasiyofaa, jambo linalohatarisha afya za wananchi na wafanyabiashara.

Alisisitiza umuhimu wa Jiji kutafuta suluhisho la kudumu, ikiwemo kuboresha mfumo wa maji taka ili kuendana na ongezeko la watumiaji.

Hata hivyo, aliwapongeza viongozi kwa kuanza mpango wa kujenga choo kipya chenye matundu 12 kitakachosaidia kupunguza changamoto hiyo, hasa katika kipindi hiki ambacho soko linatarajiwa kujengwa upya.



Pia alizungumzia changamoto ya msongamano wa magari yanayoleta bidhaa sokoni hapo, akielekeza kuwepo kwa utaratibu maalum wa magari kuingia na kushusha mizigo kwa mpangilio ili kupunguza msongamano na kuboresha usafi.




Alipendekeza magari yapaki katika maeneo maalum yaliyo nje ya soko, kisha yaingie kwa zamu kushusha bidhaa.

Katika hatua nyengine alisisitiza umuhimu wa kujenga mifereji ya maji ili kuzuia maji ya mvua kutuama au kuingia sokoni, hali inayochangia uchafu na uharibifu wa mazingira.


Alimalizia kwa kuwataka viongozi wa Jiji kuwa karibu na wananchi na kushughulikia changamoto zao kwa vitendo, akibainisha kuwa wananchi hao ndio chanzo cha mapato ya Jiji kupitia kodi.



Kwa upande wake, Naibu Meya Khalid Rashid alisema kuwa Jiji lina mpango wa kuboresha miundombinu ya ndani ya soko, ikiwemo njia za kupita ili kuondoa changamoto ya matope wakati wa mvua. Alibainisha kuwa kazi hiyo inatarajiwa kuanza ndani ya wiki moja.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com