
Neema Nkumbi, Ushetu
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Shinyanga (SHUWASA) imeshiriki katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Ushetu, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Afisa maendeleo ya jamii kutoka SHUWASA Angel Mwaipopo amesema mamlaka hiyo inaendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha wananchi, hususan wanawake na wasichana, wanapata huduma ya maji safi na salama kwa urahisi.
Ameeleza kuwa upatikanaji wa maji kwa muda wote ni hatua muhimu katika kupunguza changamoto zinazowakabili wanawake, ambao mara nyingi hubeba jukumu kubwa la kutafuta maji kwa ajili ya familia zao.
Mwaipopo amesema SHUWASA inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji katika maeneo tofauti ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa uhakika na kwa muda wote.
Aidha amesisitiza kuwa upatikanaji wa maji ya uhakika unasaidia wanawake na wasichana kutumia muda wao katika shughuli nyingine za maendeleo badala ya kutumia muda mwingi kutafuta maji.
Maadhimisho hayo yameongozwa na kauli mbiu isemayo “Haki kwa Wanawake na Wasichana: Msingi wa Maendeleo Jumuishi Kufikia Dira ya 2050.”









Social Plugin